Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

ADABU/UTARATIBU WA MAJADILIANO/MIDAHALO KATIKA UISLAMU

Faida

22. ADABU/UTARATIBU WA MAJADILIANO/MIDAHALO KATIKA UISLAMU.

Utanngulizi:

KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU.

         Sifa zote njema ni za Allah, Mola Mlezi wa viumbe vyote. Na Rehema na Amani zimshukie Bwana wetu; Mtume wa Allah na wote walio mkubali na kumfuata mpaka siku ya Kiyama.

Msomaji mwema

Assalaam Alaykum Warahmatullah Wabarakaatuh!

Baada ya kukamilika na kutamatia kwa mfululizo wa makala zetu zilizo kuwa zikikujia chini ya anuani: DA’AWAH (MLINGANO) TIMILIFU NA UKUMBUSHO ENEVU. Leo tena kwa auni na iraada yake Maulana, mtumishi wa uma; Website Uislamu, anakuletea mfululizo wa makala mpya, zitakazo kujia chini ya anuani: ADABU/UTARATIBU WA MAJADILIANO/MIDAHALO KATIKA UISLAMU. Tunataraji kwa taufiq yake Allah, makala hizi zitakunufaisha, kukuelimisha na kukufundisha khususan katika kipindi hiki ambacho kimesheheni mihadhara, midahalo na majadiliano baina ya ama waumini wa dini moja wao kwa wao au baina ya dini mbili tofauti. Au hata baina ya waumini wa dini na wale wasio waumini wa dini yoyote kama wanavyo dai, ingawa huko kutokuwa na dini ndio dini yao.

Tunasema hali ya kutaraji msaada wa Allah na hali ya kuwa Yeye ndiye Mjuzi mno:

Katika jumla ya njia/miundo hekima iliyo enda kina kimaana ambayo Qur-ani Tukufu imeitumia katika kujenga/kusimamisha hoja/dalili juu ya umoja/upweke wa Allah Ataadhamiaye. Na juu ya ukweli wa mitume watukufu katika ule ujumbe wanao wafikishia kaumu zao kutoka kwa Mola Muumba wao. Ni njia/miundo ya majibizano/mijadala/midahalo na mahojiano kwa lengo la kuifikia na kuidhihirisha haki kwa njia ya ukinaishaji akili na ubaridi nafsi. Njia ambayo humfanya mdau wake kuishi maisha yake hali ya kuwa yu thabiti/imara juu ya kile alicho kiamini, uthabiti usio kinzwa na shaka, wala kuzongwa na fikra dhanifu zisizo na mashiko.

Na pengine huenda mzizi “KAULI” na maneno (vitenzi/viarifa) vichimbukavyo katika mzizi huo, mithili ya viarifa: “amesema/alisema”, “anasema”, “sema”, “wamesema/walisema”, wanasema”, “semeni” na kadhalika. Mzizi huu wa maneno ambayo unafahamisha juu ya kujibizana/kujadiliana na kuhojiana na kuhadhirisha baina ya watu katika mambo/masuala maalumu. Umekaririka na kujirudia rudia mzizi huo na vinyambuliko vyake kwa zaidi ya mara alfu moja na mia saba. [Rejea AL-MU’UJAMUL-MUFAHRASA LIAL-FAADHWIL-QUR’AANIL-KARIYM, sahifa 554-578 ya Ustaadh Muhammad Fuad Abdul-Baaqiy-Allah amrehemu].

Kwa mfano, tamko “amesema” limekaririka zaidi ya mara mia tano, miongoni mwa mara hizo ni kauli yake Atukukiaye: “HUKUMWONA YULE ALIYE HOJIANA NA IBRAHIM JUU YA MOLA WAKE MLEZI KWA SABABU ALLAH ALIMPA UFALME? IBRAHIM ALIPO SEMA: MOLA WANGU NI YULE ANAYEHUISHA NA KUFISHA. YEYE AKASEMA: MIMI PIA NAHUISHA NA KUFISHA. IBRAHIM AKASEMA: ALLAH HULICHOMOZESHA JUA MASHARIKI, BASI WEWE LICHOMOZESHE MAGHARIBI. AKAFEDHEHEKA YULE ALIYE KUFURU; NA ALLAH HAWAONGOI WATU MADHAALIMU”. [02:258]

Na tamko “walisema” limekaririka ndani ya Qur-ani Tukufu zaidi ya mara mia tatu, miongoni mwake ni kauli yake Atukukiaye: “NA WALISEMA: HAUTATUGUSA MOTO ILA KWA SIKU CHACHE TU. SEMA: MMECHUKUA AHADI KWA ALLAH? KWELI ALLAH HATOKWENDA KINYUME NA AHADI YAKE. AU MNAMSINGIZIA ALLAH MAMBO MSIYO YAJUA?” [02:80]

Na tamko “anasema/alisema” limekaririka katika Qur-ani Tukufu mara themanini na sita, miongoni mwazo ni kauli yake Ataadhamiaye: “ILE SIKU AMBAYO ALLAH ATAKAPO WAKUSANYA MITUME AWAAMBIE: MLIJIBIWA NINI? WATASEMA: HATUNA UJUZI, HAKIKA WEWE NDIYE MJUZI MKUBWA WA YOTE YALIYO FICHIKANA”. [05:109]

Na tamko “sema” limekaririka ndani ya Qur-ani Tukufu kwa zaidi ya mara mia tatu, miongoni mwa hizo ni kauli yake Atukukiaye: “SEMA: KITU GANI USHAHIDI WAKE MKUBWA KABISA? SEMA: ALLAH. YEYE NDIYE SHAHIDI BAINA YANGU NA NYINYI. NA NIMEFUNULIWA QUR’ANI HII ILI KWAYO NIKUONYENI NYINYI NA KILA INAYO MFIKIA. ATI KWELI NYINYI MNASHUHUDIA KUWA PAMOJA NA ALLAH WAPO MIUNGU WENGINE? SEMA: MIMI SISHUHUDII HAYO. SEMA: HAKIKA YEYE NI MUNGU MMOJA TU, NAMI NI MBALI NA MNAO WASHIRIKISHA”. [06:19]

Namna/muundo wa majadiliano/mdahalo katika Qur-ani Tukufu ni wa pekee kutokana na ukunjufu wa wigo wake na uwazi wa kadhia/masuala yake na uenevu wake wa mas-ala mengi yasiyo dhibitika na mtu akayesha. Yamo mazungumzo/majadiliano baina ya Muumba Mtukufu na viumbe wake miongoni mwa mitume watukufu, malaika wakurubishwa na shetani mrujumiwa. Na yapo mahojiano au mazungumzo yanayo jiri kuhusiana na umoja/upweke wa Allah, au kuhusiana na Qur-ani Tukufu. Au kuhusiana na siku ya mwisho na yaliyomo ndani yake miongoni mwa thawabu na adhabu. Hali kadhalika yako mazungumzo/mahojiano baina ya mitume na kaumu zao, au baina ya wema na waovu, au baina ya wema wao kwa wao, au baina ya waovu na waovu wenziwao. Kama ambavyo yapo mahojiano/mazungumzo pamoja na watu wa kitabu (Mayahudi/Manaswara) au pamoja na wanafiki. Au pamoja na wageza/wafuataji wa wahenga/viongozi wao katika batili/upotofu au pamoja na wenye kumuuliza Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Na hali kadhalika yako mazungumzo au maelezo yanayo fungamana moja kwa moja na shaksiya (dhamira/dhati) ya Mtume au risala (ujumbe) yake. Au na vile alivyo vihalalisha au kuviharimisha Allah miongoni mwa vyakula, vinywaji na vinginevyo.

Na madhumuni/lengo/makusudio ya muhadhara/mdahalo/majadiliano na mazungumzo kwa mujibu wa Qur-ani Tukufu, ni:

      1.          Kuifikia haki na ilivyo ndivyo/sawa katika maudhui/mada ambayo mitazamo ya watu imetofautiana ndani yake.

      2.          Kumganda hasimu/mpinzani na kumshinda kwa njia ya kusimamisha nguvu ya hoja na kuleta dalili ya wazi na ushahidi enevu.

Na tutaona katika mfululizo wa makala hizi kwa taufiq yake Allah, kwamba Qur-ani Tukufu katika kuithibitisha haki ambayo Allah amewaamrisha waja wake kuifuata. Katika hili imetumia miundo/maelezo busara toshelezi, dalili za wazi wazi kabisa na hoja zenye nguvu zisizo wezwa kukengeukwa na asiye mlemavu wa akili. Vyote hivyo kwa pamoja vinaikinaisha akili yenye siha, matashi mema na nyoyo toharifu.

Pia tutaona kwa auni na iraada yake Allah Ataadhamiaye, ya kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alivyo fuata nyayo za   Qur-ani Tukufu. Katika kujadiliana na kuzungumza kwake na wafuasi wake wema pia walikivaa kiatu hicho hicho alicho kivaa yeye na wakaifuata njia yake kwa kuitendea kazi kauli yake Allah Ataadhamiaye: “HAKIKA NYINYI MNAYO RUWAZA NJEMA KWA MTUME WA ALLAH KWA ANAYE MTARAJI ALLAH NA SIKU YA MWISHO, NA AKAMKUMBUKA ALLAH SANA”. [33:21]

Tunamuomba Allah Atukukiaye atuwafikishe kuyatenda yale ayapendayo na kuyaridhia na aturuzuku unyoofu na utakasifu wa nia katika kauli na matendo yetu. Hakika Yeye ni Muombwa Mtukufu mno na Mtegemewa bora mno.

  

 | Tuandikie |