Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

SABABU ZA KUTOFAUTIANA MAONI BAINA YA WATU

Faida

SURA YA KWANZA

Sababu za Ikhtilafu/kutofautiana maoni baina ya watu:

         Ikhtilafu/tofauti baina ya watu katika mambo/masuala ya dini yao na katika kadhia za Dunia yao, ni suala kongwe, la tangu na tangu. Na tofauti hizi zitaendelea kuishi na kusalikia miongoni mwao mpaka kumalizika kwa Dunia na vyote vilivyomo humo. Ukweli huu usio kanushika na akili pevu na hakika hii isiyo katalika, imekokotezwa na kusisitizwa na Qur-ani Tukufu kupitia aya zake nyingi tu. Miongoni mwa hizo ni kauli yake Ataadhamiaye: “NA MOLA WAKO MLEZI ANGELI PENDA ANGELI WAFANYA WATU WOTE WAKAWA UMMA MMOJA. LAKINI HAWAACHI KUKHITALIFIANA ISIPO KUWA WALE AMBAO MOLA WAKO MLEZI AMEWAREHEMU. NA KWA HIYO NDIO ALLAH AMEWAUMBA...” [11:118-119]

Yaani – Ewe Mtume! Mwenye pupa ya kutaka kaumu yako iamini! Lau Mola wako Mlezi angeli taka kuwafanya watu wote kuwa umma mmoja, wenye kukusanyika juu ya dini ya haki, basi angeli wafanya kuwa hivyo. Hashidwi, kwani matashi yake hayana wa kuyazuia, lakini Yeye kutakata na mawi (makosa) ni kwake, hakulitaka hilo ili falsafa ya kibaya/kiovu kupambanuka na kizuri/chema idhihiri na kuonekana. Na kwa sababu hiyo basi, watu muda wa kudumu kwa Dunia hawataacha kukhitalifiana katika fikra zao, mielekeo yao, malengo yao, matarajio yao, na.......... na.......... Watakao salimika na wimbi hili la Ikhtilafu, ni wale tu walio patwa na Rehema za Bwana Mlezi wako. Basi hao wakaiongokea njia ya haki, hakika hao hawajapata kukhitilafiana katika msingi/shina lolote la dini ya haki, bali huijua njia ya haki wakaifuata.

Na tambua na ufahamu ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-kwamba hekima ya Kimungu imetaka watu wawe ni wenye kukhitalifiana. Na kwamba rehema ya Mola Mlezi wako ambayo imekienea kila kitu, itawakusanya maadam ikhtilafu zao hizo ni kwa ajili/lengo la kuifikia haki na ilivyo ndivyo.

Na ifananayo na aya tuliyo tangulia kuinukuu, ni kauli yake Atukukiaye: “...NA LAU KUWA ALLAH ANGEPENDA, ANGELI WAKUSANYA KWENYE UWONGOFU, BASI USIWE MIONGONI MWA WASIO JUA”. [06:35] – Yaani – Lau Allah Ataadhamiaye angeli taka kuwakusanya watu wote katika dini ya haki, angeli wakusanya. Lakini Yeye kutakata na mawi ni kwake, hakulitaka hilo ili apate kuwalipa wale walio tenda uovu kwa jinsi ya waliyo yatenda na awalipe mema wale walio tenda mema. Basi ewe Mtume usiwe miongoni mwa walio jingikiwa na suna/utaratibu na kanuni za Allah kwa viumbe wake.

Bali hakika Qur-ani Tukufu inaashiria kwamba kukhitalifiana watu kwa ajili ya kuinusuru haki na kueneza uadilifu, hilo ni jambo linalo lazimishwa na maslahi ya watu. Na linapelekewa na hali zao na manufaa yao. Allah Ataadhamiaye amesema: “...NA LAU KUWA ALLAH HAWAPAMBANISHI WATU KWA WATU BASI DUNIA INGELI HARIBIKA. LAKINI ALLAH NI MWENYE FADHILA JUU YA WALIMWENGU WOTE”. [02:251] – Yaani – Lau si kuwa Allah anawapambanisha wadau wa batili na wale wadau wa haki, basi bila ya shaka Dunia ingeli fisidika na ingeli enewa na maharibiko. Hii ni kwa sababu wadau wa batili watakapo achwa bila ya kupingwa, shari yao itatapakaa kote. Lakini Allah Ataadhamiaye; Mwenye fadhila kuu kwa watu wote, rehema zake zimepelekea kuwawafikisha watengenevu kupambana na mafisadi waharibifu. Na kuwapa hoja na nguvu ambazo kwa msaada wake ushindi unakuwa ni fungu la wadau wa haki dhidi ya wadau wa batili.

Twendapo sanjari na aya tukufu tuliyo inukuu, tunaikuta inawaamrisha wema katika kila zama na mahala popote, kusimama imara mbele ya waovu; wajaa shari. Na wapambane nao kwa njia yoyote ambayo dhima yake ni kuweka ukuta baina yao na fisadi na dhuluma.

Na miongoni mwa aya tukufu zilizo katika maana hii, ni kauli yake Atukukiaye: “...NA LAU KUWA ALLAH HAWAKINGI WATU KWA WATU, BASI HAPANA SHAKA ZINGELI VUNJWA NYUMBA ZA WAT’AWA, NA MASINAGOGI, NA MISIKITI, AMBAMO NDANI YAKE JINA LA ALLAH LINATAJWA KWA WINGI. NA BILA YA SHAKA ALLAH HUMSAIDIA YULE ANAYE MSAIDIA YEYE. HAKIKA ALLAH NI MWENYE NGUVU MTUKUFU”. [22:40]

Yaani – Lau kuwa si Allah Atukukiaye amewapa idhini wadau wa haki kupambana na wadau wa batili, basi bila ya shaka wadau hao wa batili wangeli eneza fisadi/maharibiko katika ardhi. Na wangeli vunja katika zama za Nabii Musa na Isa-Amani iwashukie-sehemu (nyumba) za ibada za wafuasi wao. Na wangeli vunja katika zama za Nabii Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-misikiti ambayo humo husimamishwa swala kwa Waislamu.

Kukhitilafiana baina ya watu katika masuala ya kidini na kidunia, kuna sababu nyingi na vipelekeshi vya aina mbali mbali. Miongoni mwa sababu/vipelekeshi hivyo viko vilivyo dhaahiri shahiri na ambavyo viko batini ilo fichikana. Na viko ambavyo kipelekeshi chake ni kuijua hakika kwa njia ya ukamilifu na kusimamisha hoja na dalili juu ya hilo. Na aina hii ndio inayo julikana katika Istilahi za wanazuoni wa bahathi (utafiti) kama mjadala au mdahalo.

Na katika jumla ya sababu za Ikhtilafu baina ya watu, ni kutokuwa na uwazi wa maono ya maudhui kwa pande zake zote. Huyu ufahamu na uelewa wake uko katika upande maalumu na yule ufahamu wake uko katika upande mwingine usio ule wa mwezake. Na yule wa tatu ufahamu na uelewa wake unatofautiana na ule wa mtu wa kwanza na wa pili.

Wamekwisha sema watu wenye busara zamani: Hakika haki watu hawajapata kuipatia ilivyo kwa njia zake zote na hawajapata kuikosea kwa njia zake zote. Bali baadhi yake walipatia sehemu/upande wake (hiyo haki) na wengine wakapatia upande mwingine. Wakaupigia mfano msemo wao huu, kwa hadithi ya vipofu walio muondokea tembo mkubwa. Kila mmoja kati yao akampapasa kwenye sehemu ya mwili wake na kumsifia kwa taswira aliyo isawirisha. Basi akasema yule aliye upapasa mguu wa tembo huyo mkubwa: Hakika mnyama huyu ni kama mtende mrefu. Na akasema yule aliye upapasa mgongo wa tembo huyo mkubwa: Hakika umbile lake linafanana mno na kilima kilicho inuka. Na mwingine..... na mwingine........ Namna hivi kila mmoja wao amemuelezea tembo kwa wasifu ulio guswa na mkono wake. Kwa upande huu yeye ni mkweli, lakini yeye huyo huyo kwa upande mwingine anakosea kwa kumkadhibisha mwenzake kwa wasifu alio utoa yeye ambao unakhalifiana na ule alio utoa yeye. Allah amrehemu Sheikh wetu Muhammad Abu Zahrah, hakika yeye alisema baada ya kuupiga mfano huu: “Basi angalia ni namna gani ukweli ulivyo wakusanya pamoja na angalia uwongo na makosa namna yalivyo waingia mpaka yakawatawanya”. [Rejea TAARIKHUL-JADAL, Sahifa 8, chapa ya DAARUL-Fikri AL-ARABIY, mwaka 1980]

Na aina hii ya ikhtilafu pengine ndio nyepesi kuliko zote, kwa sababu hii inatazamiwa kuondoka au kumalizika yenyewe baada ya kuijua hakika kwa ukamilifu. Na baada ya kuyajua mas-ala kwa njia zake zote na baada ya kufunguliwa mahala pa mzozo. Ni kwa ajili hii ndipo Wanazuoni wakasema: Patakapo julikana mahala pa mzozo, tofauti zote hubatilika.

Kadhalika katika jumla ya sababu za Ikhtilafu baina ya watu, ni kushikilia kumfuata mtu bila ya dalili madhubuti au hoja yenye mashiko. Na ilhali wewe unaisoma Qur-ani Tukufu na unazikuta aya zake nyingi zinawatangazia kifo waghafilika, majaahili na wapotea kwa kushikilia kwao kuwafuata na kuwaiga wahenga wao au viongozi wao. Na miongoni mwa aya zilizo pokelewa katika kulizungumzia hili, ni kauli yake Atukukiaye: “NA WANAPO AMBIWA: FUATENI ALIYO YATEREMSHA ALLAH; WAO HUSEMA: BALI TUTAFUATA TULIYO WAKUTA NAYO BABA ZETU. JE, HATA IKIWA BABA ZAO WALIKUWA HAWAELEWI KITU, WALA HAWAKUONGOKA?” [02:170] – Yaani wanapo ambiwa wale walio upendelea upotofu juu ya uwongofu: Fuateni yale Allah Ataadhamiaye aliyo yateremsha kwa Mtume wake-Rehema na Amani zimshukie-yaani Qur-ani inayo ongozea kwenye haki. Hupuuza kusikiliza nasaha na wakafikia kusema kwa inadi na upumbavu: Bali tutafuata ibada ya masanamu na kuwanyenyekea viongozi, itikadi tuliyo wakuta nayo baba zetu. Qur-ani inawarudi kwa muundo sakhiri: “...JE, HATA IKIWA BABA ZAO WALIKUWA HAWAELEWI KITU, WALA HAWAKUONGOKA?” – Yaani hawa majaahili wanawafuata baba zao na kuwaiga katika ukafiri, ufasiki na uasi hata kama baba zao hao walikuwa hawajui chochote katika masuala ya dini sahihi?! Na wala hawakuongozea kwenye njia ya haki na iliyo sawa?!

Kisha tena Qur-ani inapiga mfano wa watu hawa majaahili katika ubaya wa hali yao, inasema: “NA MFANO WA WALIO KUFURU NI KAMA MFANO WA ANAYE MPIGIA KELELE ASIYE SIKIA ILA WITO NA SAUTI, NI VIZIWI, MABUBU, VIPOFU, KWA HIVYO HAWAELEWI”. [02:171] – Yaani na mfano wa mtu anaye waita makafiri kuja kwenye njia ya uwongofu, ilhali wao wanampuuza na kujitenga mbali nae. Ni kama mfano wa mchungaji anaye wapigia kelele mbuzi na kondoo wake kuwakemea. Basi wao wanaisikia sauti yake, lakini hawayaelewi ayasemayo. Kwa mfano huu basi, hawa waghafilika ni viziwi wa kuusikia wito wa haki, ni mabubu wasio weza kumuitika mlinganiaji wa haki, ni vipofu wasio ijua njia nyoofu. Kwa hali yao hiyo basi, wao hawazielewi nasaha na maongozi yanayo elekezwa kwao.

Na mfano wa aya hii, ni kauli yake Atukukiaye: “BALI WANASEMA: HAKIKA SISI TULIWAKUTA BABA ZETU WANASHIKA DINI MAKHSUSI, BASI NA SISI TUNAONGOZA NYAYO ZAO. NA KADHAALIKA HATUKUMTUMA MUONYAJI KWENYE MJI WOWOTE ILA WATU WAKE WALIO DEKA KWA STAREHE WALISEMA: HAKIKA SISI TULIWAKUTA BABA ZETU WANASHIKA DINI MAKHSUSI, NA SISI TUNAFUATA NYAYO ZAO” [43:22-23]

Na mpetwa petwa wa maneno ni kwamba: Kuwafuata kiupofu na kibubusa mababa, viongozi na wengineo, ni katika jumla ya sababu kubwa za ikhtilafu baina ya watu. Khususan pale uigaji na ufuataji unapo kuwa ni kwa njia ya inadi, kuikataa haki na kufuata matamanio maovu.

  

 | Tuandikie |