|
Hakuna
yeyote awezaye kuthubutu
kupinga kwa kinywa kipana kuwa kuna wa kiislamu ulimwenguni
kote hii leo haukumegeka na kugawanyika vipande vipande. Kuwa leo
waislamu wamegawanyika katika makundi yenye kupingana na kushutumiana wao
kwa wao, hili ni suala lililo wazi mbele ya kila mmoja wetu na wala
halihitaji hoja na ushahidi
wa kuthibitisha kuwa lipo. Historia italishuhudia na kuliandika suala hili,
nasi waislamu wa leo tutawajibika mbele ya Mola Muumba wetu kwa kuivunja
amri yake ya umoja na mshikamano baina
yetu. Kama Ulaya imefanikiwa kuzishinda tofauti zao, ikaungana na
kuwa kitu kimoja na hata kufikia kuwa na sarafu moja chini ya akili na
fikra za binadamu. Ni kwa nini basi leo waislamu tushindwe kuungana,
kushikamana na kuwa wamoja kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume na
Makhalifa wake? Kwa nini fikra na akili za kibinadamu zimeweza
kuwangunaisha watu, amri ya Allah ishindwe kutuunganisha waislamu na kuwa
uma mmoja chini ya bendera ya “LAA ILAAHA ILLAL-LAAHU MUHAMMADUR-
RASUULULLAAH” Naam zimekuwepo juhudi za makusudi za kutaka kuuondoa uma
wa kiislamu katika janga hili la utumwa wa mfarakano na utengano, janga
ambalo limewatumbukiza waislamu katika shimo la unyonge na
udhahili. Juhudi hizi nzuri zimeshuhudiwa katika pande mbalimbali
za ulimwengu wa Kiislamu, dhima kuu ya umoja huu ni kuyaunganisha pamoja
mataifa ya Kiislamu na zile nchi zenye waislamu wengi popote pale zilipo
ulimwenguni. Mafundisho ya Uislamu yaanakiri kuwa umoja, mshikamano,
kupendana na kuhurumiana ndio msingi na nguzo kuu ya mafanikio ya uma wa
Kiislamu, bali uma wowote ule hata kama ni uma wa kikafiri, muda wa kuwa
ni wamoja na wameshikamana, kufanikiwa ni tuzo na fungu lao. Hili li
bayana katika historia, rejeeni mtaona na kuukiri ukweli huu.
Uislamu
unalingania umoja na mshikamano na unatahadharisha utengano na mfrakano,
tuitegee siko la usikivu wa kufuata kauli hii ya Allah ndani ya Qur-ani
“NA SHIKAMANENI KWA KAMBA (dini) YA ALLAH NYOTE WALA MSIACHANE…………..”
(3:103)
Hii
ni amri wa muongozo utokao kwa Mola Muweza, Muumba, wetu. Nani anaamrishwa,
bila shaka, ni sisi waja wake, nani anaongozwa ni sisi viumbe wake.
Itakuwaje kama hatukuamrika na kuufuata muongozo huu? Soma mwenyewe: (NA
ATAKAYEJIEPUSHA NA MAWAIDHA YANGU, BASI KWA YAKINI ATAPATA MAISHA YENYE
DHIKI, NA SIKU YA KIAMA TUTAMFUFUA HALI YA KUWA KIPOFU. ASEME” “EWE
WANGU! MBONA UMEMFUFUA KIPOFU NA HALI NILIKUWA NIKIONA?” (Allah) ATASEMA:
“ NDIYO VIVYO HIVYO ZILIKUJA AYA ZETU UKAZISAHAU (ukazipuuza) NA
KADHALIKA LEO UTASAHAULIWA (utapuuzwa) “ (20:124-126). Hii ndio natija
na mazao ya kukaidi na kupinga amri na muongozo wa Allah. Katika aya hiyo
ya (103) iliyomo katika sura ya (3), Uislamu unatuamrisha waislamu
tuungane, tushikamane na tuwe umma mmoja wa Kiislamu. Kigezo kikuu cha
muungano kiwe ni dini ya Allah bila ya kujali rangi, lugha na mipaka
hii ya kisiasa. Ndugu zianguni waislamu, sote tunatambua na
kukubali kuwa hakuna tofauti kubwa za msingi baina ya madhehebu ya kiislamu.
Tofauti na ikhtilafu zilizokuwepo, zilizopo na zitakazoendelea kuwepo ni
ndogo ndogo tu. Tofauti hizi zinatokana na juhudi njema za Maulamaa wema wa
Kiislamu walioyatoa muhanga maisha yao yote katika kuulewa undani zaidi wa
mafunzo ya dini yao. Allah awajaze kheri zote wanazozistahiki na ziada,
Aamiyn. Ninasema kwa kinywa kipana kabisa kwamba tofauti zinazoishi ni
ndogo ndogo tu kutokana na kujua na kuamini kuwa madhehebu yote ya
kiislamu yanaunganishwa pamoja na kiungo madhubuti cha itikadi kuu za
msingi. Ninaposema itikadi kuu za msingi simaanishi kingine zaidi ya zile
nguzo tano za Uislamu, nguzo sita za Imani na nguzo mbili za Ihsaani.
Madhehebu yote yanakiri na kuziamini nguzo zote hizi, ambazo hizi ndizo
mashina na mizizi ya Uislamu. Nguzo hizi ndizo kamba au pingu
inayotujumuisha pamoja kama uma mmoja kwa kuwa waislamu wote tunayaamini
mashina haya ni dhahiri kuwa tofauti na ikhtilafu zetu ziko kwenye mambo
madogo madogo tu ambayo tunaweza kuyamithilisha na vijitawi katika mti
mkubwa au daga katika bahari ya chewa na nyangumi. Hapa ni vema
tukajiuliza, iwapo sote kama waislamu tunang’ariwa na kuangaziwa na jua
moja (Qur-ani) na mwezi mmoja
(Hadithi), hizi nyota zinatushughulisha? Tofauti na ikhtilafu katika
matawi zilikuwepo hata wakati wake Bwana Mtume – Rehema na Amani
zimshukie, rejea historia utakubaliana nami. Hivi ndio kusema tofauti
zilikuwepo, zipo leo na zitaendelea kuwepo mpaka kiyama. Tusijidanganye
hatuwezi kuziondosha wala kuzizuia hata kidogi, lazima tukubaliane hivyo
kwa sababu hayo ndio maumbile ya Mola wetu aliyotuumbia. (NA KAMA MOLA
WAKO ANGALIPENDA, ANGALIWAFANYA WATU WOTE KUWA UMATI MMOJA (angaliwafanya
wote kufuata kitu kimoja. Lakini amewapa akili na nguvu ya kutumia akili
zao hizo watakavyo, ikiwa kwa wema au kwa ubaya (KWA HIVYO WATAENDELEA TU
KUHITILAFIANA.ISIPOKUWA WALE AMBAO MOLA WAKO AMEWAREHEMU) NA KWA (rehema)
HIYO ALLAH AMEWAUMBA (ila wenyewe tu hao wengine wamekhitari mabaya.) NA
LITATIMIA NENO LA MOJA WAKO (la kuwa ) KWELI KWELI NATAIJAZA JAHANAMU KWA
MAJINI NA BINADAMU WOTE (walio wabaya)
(11.118-119) la msingi na la kufuata baada ya kuukiri ukweli huu ni
kuchukuliana, kuvumiliana na kuheshimu jitihada njema za kila upande.
Tukiufuata kwa dhati ushauri nasaha huu, bila ya shaka mizozo, migongano
na mifarakano inayoishi miongoni mwetu itakuwa imechimbiwa kaburi
lisilofukulika hata na zana bora kabisa za kisasa. Nasi tutaishi chini ya
anga la umoja na mshikamano wa kweli wa Kiislamu kama alivyoishi Bwana
Mtume na maswahaba na makhalifa baada yake na bila ya kuwasahamu maimamu
wetu wema. Basi ndugu zanguni, ninakunasihini na kuinasihi nafsi yangu
kuwa ikhtilafu za madhehebu isiwe ndio chachu
ya kudharauliana, kuchukiana, kukufurishana na kutengana, Mwenyezi
Mungu Mtukufu anatuasa na kutuonya: “NA MTIINI ALLAH NA MTUME WAKE, WALA
MSIZOZANE (msigombane), MSIJE MKAHARIBIKIWA NA KUPOTEZA NGUVU ZENU, NA
VUMILIENI (mstahamiliane). BILA SHAKA ALLAH YU PAMOJA NA WANAOVUMILIA”
(8:46) Ndugu zanguni tusikubali kabisa kumpa adui mwanya na nafasi ya
ushindi kwa sababu ya hii mifarakano na migongano inayotawala baina yetu
leo.
Uislamu
unatutaka tuhisi furaha na machungu ya waislamu wenziwetu popote pale
walipo katika ardhi hii ya Allah, mashariki na magharibi. Sote tuwe
mithili ya mwili mmoja kama anavyotuambia Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Mfano wa waumini katika kupendana kwao, kurehemeana kwao na
kuhurumiana kwao ni kama mfano wa mwili mmoja kiungo kimoja chake (mwili)
kikiumwa, mwili mzima hushirikiana nacho katika homa na kukesha”
Bukhaariy na Muslim. Mshikamano huo wa mwili wakati sehemu yake inapoumwa
ndio mshikamano na umoja unaotaka kujengwa na umma wa Kiislamu chini ya
udugu wa Kiislamu. Qur-ani tukufu inatuambia: “KWA HAKIKA WAUMINI WOTE
NI NDUGU…………
(49:10)
Katika
kuifanyia kazi kauli hii ya Mola Mtukufu, tunamkuta Bwana Mtume – Rehema
na Amani zimshukie – alipohama Madina akiuunga udugu huu wa Kiislamu
baina ya Muhajirina na Answaar. Wakawa ni ndugu wenye kupendana na
kusaidiana katika shida na raha. Aya za Qur-ani na hadithi za Mtume juu
ya udugu ni nyingi mno kuliko unavyoweza kufikiri: “NA AKAZIUNGA NYOYO
ZAO (wakapendana wote hao maswahaba zako) HATA KAMA UNGALITOA VYOTE
VILIVYOMO ARDHINI USINGALIWEZA KUZIUNGA NYOYO ZAO, LAKINI ALLAY NDIYE
ALIYEWAUNGANISHA. HAKIKA YEYE NI MBORA NAMWENYE HIKIMA” (8: 63).
Kuna
sababu nyingi za ndani na nje ya Uislamu zilizopelekea na zinapelekea
kuvunjika kwa umoja na mshikamano baina ya
umma wa Kiislamu na kuufanya kuwa dhalili, mnyonge, usiokuwa na
nguvu hata mbele ya taifa dogo dhalimu la Israel. Sehemu kubwa ya sababu
hizi zinarejea katika kipindi kile cha ukoloni ambapo nchi nyingi za
Kiislamu zilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Magharibi. Wakoloni
walipotoa uhuru kwa nchi hizi na kurejea makwao waliacha matatizo mengi ya
kiuchumi na kisiasa. Tumeyarithi matatizo haya ambayo yamekuwa ni sababu
kuu ya kutugawa, khasa lile suala la kuwekwa kwa mipaka hii ya kisiasa
tuliyonayo hivi sasa. Mipaka hii ni zao la siasa kuu ya wakoloni wale na
hata wa leo, siasa ya “Divide and rule” yaani wagawe watu kwa misingi
ya taifa/rangi/lugha ili watawalike kirahisi. Kwa kutumia saisa hii kama
msingi, wakoloni hawa walianza kujenga matabaka baina ya watu katika
makoloni yao. Wakawapandikizia fikra za kwenda na wakati, hizi zikamfanya
kila aliyeshikamana na dini khasa Uislamu ajione kuwa amechelewa na yuko
nyuma kimaendeleo. Natija ya fikra hizi ni kuupa kisogo Uislamu na kuuweka
mbele ya macho usasa wa kwenda na wakati ambao umechangia kutufikisha hapa
tulipo hii leo. Kwa upande mwingine, wakoloni hawa walihamisha utajiri wa
nchi hizi kuupeleka kwao, wakavuruga uchumi na kuziacha katika hali ya
ufakiri wa kutupwa unaorithiwa kizazi hadi kizazi, lengo likiwa ni
kuzifanya nchi hizi kuwapigia magoti na kuwanyooshea mkono wa msaada
wakoloni hawa. Msaada huu huambatana na masharti yenye madhara kwa nchi
zetu hizi na manufaa kwao. Kwa kuwa tuna shida, basi tunakubaliana nao na
kutufanya tusiwe na sauti wala uchaguzi mbele ya wakoloni hawa. Hatuna
kinywa cha kusema hapana, bali ndiyo bwana. Hii ni miongoni mwa sababu za
nje. Ama sababu zilizomo
ndani ya waislamu wenyewe ni kuyapuuza kwao mafundisho sahihi yenye
kudhaminia mafanikio yao duniani
na akheri. Haya si mengine bali ni mafundisho ya Qur-ani na suna ya Mtume
wao.
Basi
ndugu zanguni, zindukeni na itambueni mbini hii ya adui ya kutugawa ili
atutawale atakavyo. Tuunganie na tuwe uma mmoja kama alivyotuagiza Allah.
Tuelewe kuwa huku kuwa makundi
makundi ni sehemu ya adhabu ya Mola kwetu kwa sababu ya kuutupa kwetu
muongoza wake, tusome sote na tutie akilini. (SEMA: “YEYE NDIYE MUWEZA
WA KUKULETEENI ADHABU KUTOKA JUU YENU AU KUTOKA CHINI YA MIGUU YENU, AU
KUKUVURUGENIVURUGENI (muwe) MAKUNDI (yasiyopatana) NA (muweza wa)
KUWAONJESHA BAADHI YENU JEURI YA WENZAO” TAZAMA JINSI TUNAVYOELEZA AYA (kwa
namna hii) ILI WAPATE KUFAHAMU (nao hawataki kufahamu)
(6:65).
Turudi
ndugu zanguzi katika muongozo wa Allah, tushikamane, tupendane na tuwe
wamoja, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Tuzitupitie mbali
tofauti ikhtilafu zetu tanzu na tukubaliane kutokukubaliana (lets’s agree
to disagree). Allah anatuambia. (…….NA UKIKUFIKIENI KUTOKA KWANGU
MUONGOZO, BASI ATAKAYEUFUATA MUONGOZO WANGU HUO HATAPOTEA WALA HATATAABIKA.
NA ATAKAYEJIEPUSHA NA MAWAIDHA YANGU (hayo), BASI KWA YAKINI ATAPATA
MAISHA YENYE DHIKI………”) (20: 123-124)
|