Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

UISLAMU NA MASUALA YA UZAZI-LENGO KUU LA NDOA NI KUPATA WATOTO

Faida

Uhai hautaendelea au kwa maneno mengine tunaweza kusema kwamba wanadamu hawataendelea kuwepo katika ulimwengu huu kama hakutakuwepo kuzaliana. Huku kuzaliana ndiko kutadhamini mfuatano wa kizazi (generation) baada ya kizazi Wakati Mwenyezi Mungu Mtukufu alipompa mwanadamu dhima ya kuwa Khalifa ulimwenguni hapa. Ukhalifa huu ni hadhi ya juu kabisa inayomfanya mwanadamu kuwa ni bwana na mtawala wa ulimwengu huu kupitia muongozo wa Mola Muumba wake. Sasa ili huyu mwanadamu aendelee kumtumikia Mola wake kupitia ukhalifa alioumpa kama amana na dhamana, ndipo Mwenyezi Mungu akamuwekea utaratibu na sheria ya ndoa. Jukumu la ndoa liwe ni kiwanda mama cha kuzalisha makhalifa wa Allah katika ardhi hii. Kwa hivyo basi dhima kuu ya ndoa ikawa ni kuhakikisha kuwa ukhalifa unaendelea kwa kuendelea kizazi kupitia ndoa. Kwa mantiki hii tunaona kuwa lengo mama (kuu) la ndoa ni kupata watoto ili kukiendeleza kizazi cha wanadamu. Tusome pamoja: “NA ALLAH AMEKUUMBIENI WAKE KATIKA JINSI YENU (wanadamu wenziwenu sio malaika wala majini) NA AKAKUJAALIENI KUTOKA KWA WAKE ZENU WATOTO NA WAJUKUU NA AKAKURUZUKUNI VITU VIZURI VIZURI ………..” (16:72).

Ili lengo la ndoa liweze kutimia, Mwenyezi Mungu Mtukufu akamuumbia mwanadamu huyu nguvu, msukumo na mvuto wa kimaumbile kama kichocheo. Mwanamume na mwanamke kila mmoja awe ni samaki na ulimbo wa kumnasa na kuvuta mwenziwe katika ndoa na sio katika uchafu wa zinaa. Wawili hawa wapendane katika ndoa na waendeleze  ukhalifa kupitia watoto watakaowazaa. Ni kweli usiopingika kwamba Allah Mtukufu ndiye aliyeumba jozi mbili, dume na jike katika kila kitu tuvijuavyo na tusivyovijua, AMETUKUKA ALLAH ALIYEUMBA DUME NA JIKE KATIKA (vitu) VYOTE, KATIKA VILE IOTESHAVYO ARDHI, NA KATIKA NAFSI ZAO (wanadamu) NA KATIKA VILE WASIVYOVIJUA”  (36:36)

Akaliumba tone la manii katikati ya mifupa ya mgongo wa baba na kifua (mbavu) za mama. Akaliumbia tone hili mishipa na kuliandalia mapito. Akaliumbia tumbo la uzazi kuwa ndio mahala pake pa utulivu na hifadhi yake: “NA KWA YAKINI TULIMUUMBA MWANADAMU KWA UDONGO ULIO SAFI. KISHA TUKAMUUMBA KWA TONE LA MANII (mbegu ya uzazi) LILILOWEKWA KATIKA MAKAO YALIYOHIFADHIKA  KISHA TUKALIFANYA TONE HILO KUWA PANDE LA DAMU, NA TUKALIFANYA PANDE LA  DAMU HILO KUWA PANDE LA NYAMA, KISHA TUKALIFANYA PANDE LA NYAMA HILO KUWA MIFUPA, NA MIFUPA TUKAIVIKA NYAMA, KISHA TUKAMFANYA KIUMBE KINGINE ……………(23: 13-14)

Huyu ndio mwanadamu aandikaye leo makala haya na wewe uyasomayo na hizo ndizo hatua za kuumbwa kwake hata leo akafikia hapo alipo. Yote haya yanashuhudia mradi na makusudio ya Muumbaji Muweza aliyetuumba sisi viumbe wake. Mumbaji huyu asiyeshindwa na chochote bali yeye ndiye Mshindi Mtukuka analifumbuliza lengo la ndoa kupitia ulimi wa Mtume wake Rehema na Amani zimshukie: Oaneni mzaane mtaongezeka (mtakuwa wengi) kwani hakika mimi nitajifakharisha kwa nyumati kwa sababu yenu siku ya Qiyamah”  Al-baihaqy.  Ni kutokana na sababu zote hizi ndio sheria ya kiislamu ikalifanya ni hatia kubwa kosa la  kuwaua watoto: “  WALA MSIWAUE WATOTO WENU KWA KUOGOPA UMASIKINI SISI NDIO TUNAOWARUZUKU WAO NA NYINYI (pia) KWA YAKINI KUWAUA NI KHATIA KUBWA”  (17: 31)

Kosa hili la uuaji wa watoto limekuwa ni khatia kubwa kwa sababu linapelekea kutokuendelea kizazi cha wanadamu. Kauli jumla, ndoa ndio utaratibu Allah aliowawekea wanadamu wazaane na kuuendeleza ukhalifa aliowapa katika ulimwengu huu.  Kwa kauli hii hatuna hatia kusema kuwa lengo mama la ndoa ni kupata watoto, japokuwa yako malengo tawi mengine.

MTOTO NI NEEMA

Tumesema na tunasema tena kwamba kuishi milele na kubakia daima katika dunia hii ni tabia na mapenzi yaliyomo ndani ya mwanadamu. Sasa ikiwa hakuna njia wala hila ya kumuwezesha kubakia milele ulimwenguni hapa kwa dhati yake mwenyewe bali hata kuishi kwa miongo kadhaa na muhali wa hili anauona na kuishuhudia kupitia wahenga wake, Ni jinsi gani watu waliomzunguka wanavyouacha ulimwengu hali ya kuwa bado wanaupenda mmoja baada ya miwingine ili neno la Allah litimie: “KILA NAFSI ITAONJA MAUTI……….” (3: 185)

KILA KILICHO JUU YAKE (ardhi na mbingu) KITATOWEKA (kitaondoka) INABAKI DHATI YA MOLA WAKO (tu mwenyewe) MWENYE UTUKUFU NA HESHIMA” (55; 26-27)

Kutokana na neno hili la Allah lililokwishahukumiwa litimie na ambalo kiumbe mwanadamu hana uwezo, nguvu wala hila za kuliepuka au kulizuia lisitimie kwake. Mwanadamu huyu akaona njia pekee itakayomuwezesha kuendelea kuishi na kutajwa hata baada ya kifo chake ni kupitia kizazi atakachokiacha nyuma yake. Kizazi hiki kitaendelea kunasibishwa na yeye na jina lake kuendelea kuishi kwa miongo kadhaa. Ni kwa ajili hi tunawaona/tunasoma kwamba manabii na mitume wa Allah - Rehema na Amani ziwashukie wote. Walitamani kupata watoto wema. Watoto wema ambao watakuwa ni alama ya kuendelea kuwepo  kwao na kutajwa vema. Huyu hapa Nabii Ibrahim - Rehema  na Amani zimshukie akiinua mikono yake juu kwa unyenyekevu mkubwa anamuomba Mola wake mtoto mwema, anasema: EWE MOLA WANGU WEE! NIPE (mtoto awe) MIONGONI MWA WATENDA MEMA” NDIPO TUKAMPA HABARI NJEMA YA (kuwa atapata) MTOTO MPOLE. (basi akampata , naye ndiye Nabii Ismail)”  (37: 100-101).

Na huyu hapa ni Nabii Zakaria - Amani imshukie akimuomba Mola wake amruhusu kizazi chema kitakachobeba jukumu la kufikisha ujumbe wa Allah baada yake, anasema (PALE PALE ZAKARIA AKAMUOMBA MOLA WAKE AKASEMA: MOLA WANGU! NIPE KUTOKA KWAKO MTOTO MWEMA. WEWE NDIYE USIKIAYE  MAOMBI ( ya wanakuomba)” (3: 38)

“………………BASI NIPE MRITHI (anijie) KUTOKA KWAKO, ATAKAYENIRITHI (ilimu yangu na uwongozi yangu) NA KUWARITHI (wazee wake wengine) KIZAZI CHA YAAKUBU. NA UMFANYE, MOLA WANGU, MWENYE KUKURIDHISHA”  (19: 5-6)

Allah  akaisikia dua na maombi ya mja wake huyu mwema na kumjulisha hilo kupitia bishara ya malaika, MARA MALAIKA WAKAMLINGANIA, HALI AMESIMAMA AKISWALI CHUMBANI, KWAMBA ALLAH ANAKUPA KHABARI NJEMA ZA (kuwa utazaa mtoto, umuite) YAHYA, ATAKAYEKUWA MWENYE KUMSADIKISHA (Mtume atakayezaliwa) KWA NENO LITOKALO KWA ALLAH (naye ni Nabii Issa) NA ATAKAYEKUWA BWANA KABISA NA MTAWA NA NABII ANAYETOKANA NA WATU WEMA” (3: 39)

Hawa hapa waja wa Allah awapandao nao wanampenda wakimnyenyekea Mola wao na kumuomba awape burudani ya macho kutoka kwa wake na watoto wao: ‘NA WALE WANAOSEMA MOLA WETU TUPE KATIKA WAKE ZETU NA WATOTO WETU YABURUDISHAYO MACHO (yetu/nyoyo zetu) NA UTUJAALIE KUWA WAONGOZI KWA WAMCHAO ALLAH: (25: 74).

Allah Mtukufu anatuonyesha dhahiri nafasi aliyonayo mtoto anapomtumia katika kiapo chake kitukufu na kumuunganisha pamoja na mji mtukufu na Mtume wa mwisho, ansema: “NAAPA KWA MJI HUU (wa Makkah) NAWE UTASHUKA (utateremka) KATIKA MJI HUU (ambao wamekutoa na utahalalishiwa). (na ninaapa) KWA KILA KILICHOZAA NA KILAKILICHOZALIWA ( 90:13)


TUJIFUNZE NA TUKUBALI: KUWA kuzuia uzazi / kumuua mtoto ni kuizuia/kuiua neema ya Allah: ……….BASI JE, WANAZIKATAA NEEMA ZA ALLAH? (16: 71).

 


Forum | Guestbook | Tuandikie |