|
Na mahala pengine tunaiona aina nyingine ya mdahalo/majadiliano
yaliyo jiri baina ya Mtume Shuaib-Amani imshukie-na kaumu yake. Na
majadiliano haya yamekuja kwa sura yenye ufafanuzi zaidi kuliko yale
yaliyo tangulia, hebu yasikilize kupitia kauli yake Allah Ataadhamiaye:
“NA KWA WATU WA MADYANA TULIWATUMIA NDUGU YAO SHUA’IB AKASEMA: ENYI WATU
WANGU! MUABUDUNI ALLAH. NYINYI HAMNA MUNGU ILA YEYE, WALA MSIPUNGUZE
VIPIMO NA MIZANI. MIMI NAKUONENI MMO KATIKA HALI NJEMA, NAMI
NAKUKHOFIENI ADHABU YA SIKU KUBWA HIYO ITAKAYO KUZUNGUKENI. NA ENYI WATU
WANGU! TIMIZENI VIPIMO NA MIZANI KWA UADILIFU WALA MSIWAKHINI WATU VITU
VYAO; WALA MSIENEZE UOVU KATIKA NCHI MKAFANYA UHARIBIFU. ALIVYO
KUBAKISHIENI ALLAH NDIYO BORA KWA AJILI YENU, IKIWA NYINYI NI WAUMINI.
WALA MIMI SIYE MLINZI WENU”. [11:84-86]
Ndugu
msomaji-Allah akurehemu-bila ya shaka unaona ya kwamba Mtume
Shuaib-Amani imshukie-baada ya kuwaamrisha watu wake kumuabudu Allah
Ataadhamiaye peke yake. Na baada ya kuwakataza kupunja katika vipimo na
mizani, akawabainishia sababu ambazo zilizo mpelekea
kuwaamrisha/kuwakataza, akasema: Hakika mimi ninakuoneni nyinyi
mnamiliki mali nyingi, na aliye hivyo basi lililo la wajibu kwake ni
kumpa kila mwenye haki, haki yake. Nami ninakucheleeni iwapo mtaendelea
na ushirikina wenu na upunjaji wenu katika vipimo na mizani, kufikwa na
adhabu ya siku yenye vishindo vikuu. Na adhabu ya siku hiyo ni yenye
kumzunguka kila dhaalimu, mjaa madhambi.
Kisha
Mtume Shuaib-Amani imshukie-akaendelea kuwanasihi watu wake,
akawasisitizia yale aliyo kwisha kuwaamrisha katika twaa (utii kwa
Allah) na yale aliyo kwisha wakataza miongoni mwa mabaya na ya hovyo. Na
akawaongoza ya kwamba kile wanacho bakishiwa na Allah katika mali ya
halali, hicho ndicho bora kwao kuliko mali ya haramu ijapo kuwa nyingi
kiasi gani. Basi ni juu yao wao kumuitika katika hayo, iwapo wao ni
katika wale waaminio haki na uadilifu. Naye aliwaambia nasaha zote alizo
waambia, ili kujitoa katika dhima na kwa kuitekeleza amri ya Mola Mlezi
wake ambayo ni kufikisha tu. Na hesabu ya kila aliye chupa mipaka na
akafanya dhulma na akayafadhilisha mno maisha ya Dunia, iko kwa Allah
Ataadhamiaye.
Na
atakaye zisoma kwa makini aya hizo, ataona ya kwamba Mtume Shuaib-Amani
imshukie-amewaongoza watu wake kwenye yale yanayo wafaa katika imani yao
na miamala yao ya kimaisha. Na katika mahusiano/mafungamano yao wao kwa
wao, na katika mienendo yao binafsi. Amewaongozea kwenye yote hayo, kwa
muundo hekima, ulio kusanya kila kiletacho mafanikio na kuongozea kwenye
haki. Basi je, unafikiri jawabu la watu wake lilikuwa ni nini?
Hakika
jibu rejezi lao lilikuwa limesheheni kumcheza shere na kumbeza, kwa
ushahidi wa kauli yake Allah Ataadhamiaye: “WAKASEMA: EWE SHUA’IB! NI
SWALA ZAKO NDIZO ZINAZO KUAMRISHA TUYAACHE WALIYO KUWA WAKIYAABUDU BABA
ZETU, AU TUACHE KUFANYA TUPENDAVYO KATIKA MALI ZETU? AMA HAKIKA WEWE NI
MSTAHAMILIVU KWELI NA MWONGOFU!” [11:87]
Yaani:
Kaumu ya Shuaib walimwambia Mtume wao kwa njia/namna ya majivuno na
kucheza shere: Ewe Shuaib! Hivi ni hizo swala zako unazo dai kuwa Mola
wako amekuamrisha na ambazo wewe unazikithirisha, ndizo zinazo kuamrisha
tuache kuyaabudu masanamu yaliyo kuwa yakiabudiwa na baba zetu! Na ndizo
hizo zinazo kuamrisha utuambie: Acheni kupunguza katika vipimo na
mizani, na ilhali hiyo ndio ada tuliyo izoea na wala hatuwezi kuihepa!
Iwapo swala zako hizo ndizo zinazo kuamrisha utuambie hayo, basi hizo ni
swala batili na si chochote wala lolote kwetu. Lakini sisi tunaziona ni
aina mojawapo ya wazimu na usema hovyo wako.
Na
sentensi “AMA HAKIKA WEWE NI MSTAHAMILIVU KWELI NA MWONGOFU”, ni ziada
ya ucheza shere na ujivuni wao kwa Mtume wao, kama kwamba wao
wanamwambia: Unathubutuje kutuamrisha kuacha kuyaabudu masanamu na
tuache kupunguza katika vipimo na mizani, pamoja na kujua kwako kwa
yakini ya kwamba mambo mawili hayo ndio tumeyajenga maisha yetu juu
yake. Pamoja na kudai kwako kwetu ya kwamba wewe ni mstahamilivu kweli
anaye ziangalia kwa utuvu hukumu zake. Tena ni mwongofu ambaye anaye
waongoza wengine kwenye yale yanayo wanufaisha?! Hakika sifa mbili hizi
si lahiki na stahiki yako, maadam unatuamrisha hayo. Na hakika si
vinginevyo, lililo lahiki yako ni vinyume vyake, yaani ujinga na ufasiki
na uharaka katika hukumu.
Hivyo
ndivyo madhaalimu wajivuni wale walivyo mrudi Mtume na Muongozi wao;
Shuaib-Amani imshukie-naye ndiye khatibu wa Mitume, akiupuuzilia mbali
usafihi wote huo. Kwa kuwa yeye anahisi ya kwamba watu wake ni
majaahili, kama anavyo ihisi nguvu ya haki aliyo waletea kutoka kwa Mola
wake Mlezi, ndipo anapo warudi kwa kauli yake: “ENYI WATU WANGU!
MWAONAJE IKIWA NINAYO DALILI WAZI INAYO TOKANA NA MOLA WANGU MLEZI, NA
IKAWA YEYE AMENIRUZUKU RIZIKI NJEMA KUTOKA KWAKE? WALA MIMI SIPENDI
KUKUKHALIFUNI NIKAFANYA YALE NINAYO KUKATAZENI. SITAKI ILA KUTENGENEZA
KIASI NINAVYO WEZA. NA SIPATI KUWEZESHWA HAYA ILA NA ALLAH. KWAKE YEYE
NINATEGEMEA, NA KWAKE YEYE NAELEKEA. NA ENYI WATU WANGU! KUKHALIFIANA
NAMI KUSIKUPELEKEENI HATA MKASIBIWA KAMA WALIVYO SIBIWA WATU WA NUHU, AU
WATU WA HUD, AU WATU WA SALEH. NA WATU WA LUT’ SI MBALI NANYI. NA OMBENI
MSAMAHA KWA MOLA WENU MLEZI, TENA TUBUNI KWAKE. HAKIKA MOLA WANGU MLEZI
NI MWENYE KUREHEMU NA MWENYE UPENDO”. [11:88-90]
Yaani:
Mtume Shuaib-Amani imshukie-aliwaambia watu wake: Enyi watu wangu! Hebu
niambieni, lau mimi nitakuwa na hoja/dalili ya wazi, uoni/ujuzi uangazao
nilio tunukiwa na Mola wangu Mlezi, aliye Mmiliki wa yangu yote. Na
akaniruzuku riziki njema kutokana na fadhila zake, baada ya fadhila zote
hizo, hivi mnaona mimi ninafaa kufuata matamanio/matashi yenu?! Hapana,
na katu sitayafuata matashi yenu hayo, bali nitaendelea na njia yangu
hii mpaka niufikishe ujumbe wa Mola wangu Mlezi. Kisha anawafichulia
mwenendo wake pamoja nao, anawaambia: Na si sehemu ya hulka yangu mimi
kukukatazeni nyinyi kutenda jambo fulani, kisha mimi nikalitenda hilo
hilo. Na hakika si vinginevyo, mimi ninalo litaka katika haya ninayo
kuamrisheni na yale ninayo kukatazeni, ila ni kwa msaada na auni yake
Allah. Kwani ni Yeye peke yake ndiye ninaye mtegemea katika mambo yangu
yote.
Halafu
Mtume Shuaib-Amani imshukie-anaendelea kuinasihi kaumu yake,
anawagurishia kwenye kuwakumbusha maanguko ya walio tangulia.
Akiwatahadharisha usije ukawa mwisho wao kama ule mwisho wa madhaalimu
wa kabla yao, anawaambia: Enyi watu wangu! Uadui wenu kwangu
usikupelekeeni kunizulia uwongo na kuendelea kuniasi na kunipiga vita.
Kwani hilo litakupelekeeni kusibiwa na adhabu kama ile iliyo ipata kaumu
ya Nuhu, au kaumu ya Hud au kaumu ya Saleh. Na ikiwa nyinyi hamuwaidhiki
na hayo yaliyo zisibu kaumu zilizo tangulia, basi hebu waidhikini na
kaumu Lut ambao walishukiwa na adhabu, wao na mji wao. Ardhi yao
ikapinduliwa juu chini, chini juu, na wala wao hawako mbali nanyi, si
kizama wala kikanda.
Kisha
baada ya nasaha na majadiliano yote hayo, ndipo akawafungulia mlango wa
matumaini ya kupata rehema za Allah Ataadhamiaye, iwapo tu wao watatubu
na kurejea kwa Mola wao, akasema: Na mtakeni maghufira Mola wenu Mlezi
kutokana na madhambi yote mliyo yatenda na kisha tubieni kwake toba ya
kweli. Allah-utakati wa mawi ni wake-atakutakabalieni toba yenu, kwani
Yeye ni Mrehemevu mno kwa waja wake na ni Mwingi mno wa mapenzi kwa yule
anaye mtii.
Kama
hivi tunamuona Mtume Shuaib-Amani imshukie-akiipa kaumu yake aina kwa
aina za nasaha na mawaidha bali mbali na akiwazungusha katika uringo wa
uraghibishi na ukhofishi. Na akijadiliana na kuhojiana nao kwa miundo
mbali mbali. Lakini wapi, kaumu yake ilikuwa imesha fikia kileleni mwa
ufisadi, wakamrudi kwa kauli yao, kama walivyo nukuliwa na Qur-ani
Tukufu: “WAKASEMA: EWE SHUA’IBU! MENGI KATIKA HAYO UNAYO YASEMA
HATUYAFAHAMU. NA SISI TUNAKUONA HUNA NGUVU KWETU. LAU KUWA SI JAMAA ZAKO
TUNGE KUPIGA MAWE, WALA WEWE SI MTUKUFU KWETU”. [11:91]
Yaani:
Watu wa Shuaib walisema katika kumrudi Mtume wao: Ewe Shuaib! Hakika
sisi hatuyajui mengi katika hayo unayo yasema, kwani hayo ni maneno
ambayo hatujayazoea na kamwe hayatakubaliwa na nafsi zetu. Na umesha
fanya nasi midahalo mingi mpaka tunakuchukia na wala hatutaki kukuona,
nasi tunakuona wewe ni mtu dhaifu tu kwetu, usiye na ubavu wa kupambana
nasi iwapo tutataka kukufukuza katika mji wetu. Na lau kuwa si
jamaa/ndugu zako ambao wao wako pamoja nasi katika dini yetu, tungeli
kupopoa kwa mawe ukafilia mbali. Na wewe kwetu si mtu mtukufu na
hupendwi, bali kwetu sisi wewe ni mtu dhaifu, mkataliwa achukiwaye.
Hapo
sasa ndipo tunamkuta Mtume Shuaib-Amani imshukie-akigura kutoka katika
muundo wa mazungumzo laini na watu wake, na kuingia kwenye muundo wa
ukali na ukanyi wa upole. Ili kuulinda/kuutetea utukufu wa Mola wake
Mlezi, anawaambia: “ENYI WATU WANGU! KWANI JAMAA ZANGU NI WATUKUFU ZAIDI
KWENU KULIKO ALLAH? NA YEYE MMEMUEKA NYUMA YA MIGONGO YENU! HAKIKA MOLA
WANGU MLEZI NI MWENYE KUYAZUNGUKA YOTE MNAYO YATENDA. NA ENYI WATU
WANGU! FANYENI MWEZAYO, NA MIMI PIA NINAFANYA. KARIBUNI MTAJUA NI NANI
ITAKAYE MFIKA ADHABU YA KUMHIZI, NA NANI ALIYE MWONGO. NA NGOJENI, NAMI
PIA NINANGOJA PAMOJA NANYI”. [11:92-93]
Yaani:
Mtume Shuaib-Amani imshukie-aliwaambia watu wake kwa ghadhabu kwa ajili
ya kuilinda dini na itikadi yake dhidi ya kudharauliwa: Hivi ni kwa
sababu tu ya ndugu na jamaa zangu ndio hamkunipopoa mawe, hao ndio bora
na watukufu kwenu kuliko Allah ambaye Yeye ndiye Muumba wenu, Mpa riziki
wenu, Mfishaji na Mpa uhai wenu. Na ambaye mmeyafanya maarimsho na
makatazo yake niliyo kuleteeni kutoka kwake, kuwa ni kitu kitupwacho
kisicho na punje ya thamani! Hakika Mola wangu Mlezi ameyazunguka kwa
kuyajua fika maneno yenu hayo na kauli zenu hizo na atakulipeni adhabu
fedheheshi iliyo stahiki yenu. Na enyi watu wangu nyie! Tendeni lolote
mnalo weza kunitendea na nitisheni na nikamieni mtakavyo, yote hayo
hayatanidhuru hata ukucha. Yatawezaje kunidhuru na ilhali mimi
ninamtegemea Allah Mtegemewa wa msaada na uangalizi/ulinzi wake?! Nami
sitayakabili matendo yenu hayo maovu kwa uovu, bali nitayarudi kwa
matendo mema nako ni kule kukuiteni kwenye upweke wa Allah Ataadhamiaye
na kwenye tabia njema. Na punde tu mtajua ni nani baina yetu nanyi
atakaye fikwa na adhabu itakayo mfedhehesha na kumdunisha. Na ni nani
miongoni mwetu aliye muongo katika kauli na matendo yake. Na ngojeeni
mwisho mbaya kwa kunikadhibisha, nami ninangojea pamoja nanyi. Mtume
Shuaib-Amani imshukie-hakungojea muda mrefu, kwani iliwafikia kaumu yake
walio madhaalimu, adhabu iliyo wadamirisha (walihikisha) kabisa.
|