|
UMUHIMU WA WAKATI KWA MUISLAMU….(i)
Wakati ni suala
lenye umuhimu wa pekee katika maisha ya muislamu. Umuhimu huu unatokana na
mtizamo wa Uislamu kwa wakati kuwa ndio maisha/uhai wenyewe. Kwani hizi
sekunde,dakika, saa, siku,juma,mwezi na hatimaye mwaka hazimaanishi ila
umri wa mwanadamu na kumalizika kwake. Uislamu unaithamini na kuidhibiti
kila dakika inayompitia mwanadamu na umemuwekea dhana ya kuhesabiwa juu ya
dakika yake hiyo ambayo haiwakilishi ila uhai wake. Huu ndio mtizamo na
msimamo wa Uislamu kuhusiana na suala zima la wakati;mtizamo unaokinzana
na mtizamo wa wale wanaodai kuwa ni waislamu,khususan waislamu wa leo.
Waislamu wa leo wanashindana katika kuupoteza pasipo na faida wakati wao
kwa njia mbalimbali. Ushindani huu ndio uliozaa msemo shahiri utumikao
leo, ambapo utamsikia mtu anasema: (Naenda kupoteza wakati). Msemo huu
haumaanishi ila ni kuwa muhusika ana wakati (muda) kifaya(tosha) kuliko
mahitaji yake, kiasi cha kutokujua autumieje huo muda wake wa ziada. Hapo
ndipo huamua kwenda kijiweni kwa wale vijana au kwenye baraza ya
kahawa/karata/bao kwa wale wazee. Hivi kweli inamkinika kwa muislamu
kuutumia hivi wakati wake na il-hali kitabu chake kitukufu ndicho
kinachosema kwa ndimi za watu waovu watakaposema siku ya kiyama. Baada ya
kupewa vitabu vya amali zao: “NA MADAFTARI YATAWEKWA(mbele yao).
UTAWAONA WABAYA WANAVYOOGOPA KWA SABABU YA YALE YALIYOMO (madaftarini) NA
WATASEMA: OLE WETU! (Ee kuangamia kwetu leo!) NAMNA GANI MADAFTARI HAYA!
HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)! NA WATAKUTA
YOTE YALE WALIYOYAFANYAYAMEHUDHURIA HAPO, NA MOLA WAO HAMDHULUMU YO
YOTE”. [18:49]
Yatakayokuwamo
ndani ya madaftari ya amali ya waja siku ya hesabu na malipo (kiyama) ni
natija ya namna walivyoitumia neema ya wakati (uhai) waliopewa bure na
Mola Muumba wao. Hapo ndipo unapodhihiri umuhimu wa wakati katika maisha
ya muislamu bali mwanadamu. Kumbuka ewe ndugu muislamu (Allah akuzindue)
wakati ambapo wewe unauchezea na kuupoteza wakati (uhai) wako katika mambo
yasiyokunufaisha bali kukudhuru.madola makuu (mataifa ya kikafiri)
yanahakikisha kuwa yanaitumia vyema kila fursa ya dakika waipatayo
kuitawala anga na bahari. Lengo kuu likiwa ni kukutawala wewe muislamu
kijeshi, kiuchumi, kielimu, kiutamaduni,kifikra na hata ikiwezekana
kiitikadi pia.
Hebu pekua
kurasa za historia (tarekh) uone ni jinsi gani waislamu wa mwanzo
walivyojua umuhimu wa wakati (uhai). Na namna walivyoupa thamani yake na
wakati ukawathamini na kuwapa thamara (matunda) yake. Miongoni mwa thamara
hizo ni elimu yenye manufaa inayotunufaisha hata sisi leo,amali njema
zilizowahakikishia utukufu na daraja za juu mbele ya Mola wao na ulimwengu
mzima wa kiislamu muda wa
kusalikia mbingu na ardhi. Jihadi yenye kukubaliwa na Allah iliyoueneza
Uislamu mashariki na magharibi. Ni kutokana na jihadi yao hiyo njema
ndio na akina sisi tukapata bahati ya kuwa waislamu-Alhamdulillah!
Ustaarabu uliowabakishia utu na ubinadamu wao hata wakawa ni kigezo kwa
watu wa jamii nyingine na nembo yao ikawa ni ile dua iliyosajiliwa na
Qur-ani: “…MOLA WETU! TUPE MEMA DUNIANI NA (tupe) MEMA AKHERA, NA
UTULINDE NA ADHABU YA MOTO”. [2:201]
Haya ni baadhi
tu ya matunda waliyoyapata waislamu wa mwanzo kutokana na kuuthamini na
kuutumia vema wakati.
QUR-ANI NA
SUNAH (HADITHI) ZINAVYOUTHAMINI NA KUUSHUGHULIKIA WAKATI.
Kabla
hatujaanza kuliangalia hili kwa pamoja, ni vema tukafahamu kwamba Uislamu
unamtaka muislamu aushughulikie ulimwengu wake huu aishimo leo kama kwamba
ataishi milele, hatokufa abadan. Maana na tafsiri sahihi ya agizo hili
la Uislamu ni kuwa muislamu ajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili
aishi maisha mazuri na asiwe tegemezi na mzigo kwa jamii. Maisha ambayo
yatamuhakikishia kupata mahitaji yake yote ya lazima; ale, anywe , alale
mahala pazuri na apate elimu bora sambamba na uhuru wa kuabudu kwa mujibu
wa dini yake. Huu ni upande mmoja, kwa upande wa pili Uislamu unamuagiza
muislamu kuishughulikia akhera yake, mahala ambako ndiko yaliko maisha
yake ya milele, kama kwamba atakufa kesho. Tafsiri safi ya agizo hili ni
kuwa muislamu anatakiwa asighurike na dunia ipitayo kiasi cha kuisahau
akhera iliyo makazi yake ya milele.
Baada ya
kukumbushana juu ya agizo hili la Uislamu; dini ya maumbile, hebu sasa na
tuanze kuiangalia Qur-ani Tukufu inavyoutazama wakati na umuhimu wake,
tusome na tuzingatie pamoja: “NA AKAKUTIISHIENI JUA NA MWEZI, MAISHA YAO
(yanafanya yaliyoamrishwa ya kuchomoza na kuchwa na mengineyo kwa ajili ya
manufaa yenu) NA AKAKUTIISHIENI MCHANA NA USIKU NA AKAKUPENI KILA
MLICHOMUOMBA (na msichomuomba). NA KAMA MKIHISABU NEEMA ZA ALLAH,
HAMTAWEZA KUZIHISABU…” [14:33-34]
Hapa Allah Mola
Mtukufu anamkumbusha mwanadamu kuwa miongoni mwa neema zake nyingi
alizomneemesha ni pamoja na neema ya jua na mwezi. Neema mbili hizi ndizo
mihimili mikuu na chanzo cha kuhesabia wakati ambacho hutupatia usiku na
mchana. Allah anazidi kutukumbusha juu ya neema hii ya wakati, hebu
tumtegee sikio la usikivu: “NAYE NDIYE ALIYEFANYA USIKU NA MCHANA
UFUATANE KWA (nafuu ya yule) ANAYETAKA KUKUMBUKA AU ANAYETAKA KUSHUKURU
(atatanabahi kwa kuja na kuondoka kwa mchana na usiku)”. [25:62]
Mfuatano wa
mchana na usiku; yaani usiku ukaondoka na mahala pake pakachukuliwa na
mchana na kinyume chake ni katika jumla ya neema za Allah zilizo kwa
mwanadamu. Haukuwa usiku na mchana ila ni wakati ambao humpa mwanadamu
fursa ya kufanya amali zitakazomdhaminia kheri na mafanikio ya ulimwengu
huu na ule ujao. Nafsi ya kufuatana kwa mchana na usiku hakupungui kuwa ni
neema ambayo mwanadamu anawajibika kuishukuru. Kwani kila kimoja mbali ya
kuwa kwake ni wakati (uhai)
kina jukumu na manufa yake kwa mwanadamu ambayo mwenzake hawezi
kuyatekeleza. Lau ingelikuwa ni usiku tu milele bila ya mchana au ni
mchana daima bila ya usiku, maisha yangelimwia uzito mwanadamu, bali
yasingeliwezekana kamwe. Na hii ndio sehemu tu ya hekima na falsafa ya
kauli tukufu ya Allah: “SEMA: NIAMBIENI, KAMA ALLAH AKIUFANYA USIKU
UKUKALIENI MOJA KWA MOJA MPAKA SIKU YA KIYAMA, NI MUNGU GANI ASIYEKUWA
ALLAH ATAKAYEKULETEENI MWANGA? BASI JEE, HAMSIKII? SEMA: NIAMBIENI, KAMA
ALLAH AKIUFANYA MCHANA KUKUKALIENI MOJA KWA MOJA MPAKA SIKU YA KIYAMA, NI
MUNGU GANI ASIYEKUWA ALLAH ATAKAYEKULETEENI USIKU MNAOPUMUA HUMO? BASI JE,
HAMUONI (ihsani za Allah)? NA KWA REHEMA ZAKE AMEKUFANYIENI USIKU NA
MCHANA ILI MPUMUE HAPO USIKU NA MTAFUTE FADHILA ZAKE (hapo mchana) NA ILI
MPATE KUSHUKURU”. [28:71-73]
Katika
kuuonyesha umuhimu wa wakati Allah ameapa mianzoni mwa sura mbalimbali
zilizoshuka Makkah kwa wakati au sehemu ya wakati, mithili ya kauli hizi:
“NAAPA KWA USIKU UFUNIKAPO (kila kitu) NA KWA MCHANA UANGAZAPO”.
[89:1-2]
“NAAPA KWA
MCHANA NA KWA USIKU UNAPOTANDA”. [93:1-2]
“NAAPA KWA
ZAMA (zako ewe nabii Muhammad) KUWA BINADAMU YUKO KATIKA KHASARA”.
[103:1-2]
Inajulikana
kutokana na elimu ya tafsiri kwamba Allah Mteremshaji wa Qur-ani Tukufu
anapoapa kwa cho chote miongoni mwa viumbe vyake. Hufanya hivyo ili kuvuta
fikra na mtazamo wa waja wake kukielekea kitu hicho alichokiapia na
wautanabahi utukufu, manufaa na athari ya kitu hicho katika maisha yao ya
kila siku.
Suna ya
Mtume-Rehema na Amani zimshukie- haikubakia nyuma katika kusisitiza na
kuonyesha thamani ya wakati. Na jinsi mwanadamu atakavyowajibika mbele ya
Allah siku ya kiyama kuhusiana na neema hii ya wakati aliyopewa
aliitumiaje. Hata ikawa miongoni mwa maswali manne ya msingi atakayoulizwa
mja siku hiyo ya hesabu, mawili yanahusika moja kwa moja na wakati.
Imepokelewa kutoka kwa Muaadh Ibn Jabal-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-
Rehema na Amani zimshukie- amesema: “Hazitaondoka nyayo (miguu) za mja
siku ya Kiyama (kuingia peponi/motoni)mpaka aulizwe mambo manne:
i.
Umri wake ameumaliza katika mambo gani.
ii.
Ujana wake ameuchakaza katika mambo gani.
iii.
Mali yake ameichuma katika njia gani (za halali/haramu) na
aliitumiaje.
iv.
Na elimu yake ameifanyia nini”.
Bazzaar &
Twabaraaniy
Hivi ndivyo
atakavyoulizwa mwanadamu kuhusiana na umri wake kwa ujumla na khasa ujana
ambao ni sehemu ya huo umri. Kwa nini ujana na sio utoto au uzee? Hili
linatokana na umuhimu wa kipindi cha ujana katika umri mzima wa mwanadamu.
Kipindi hiki kina nafasi na thamani ya pekee katika uhai wote wa mwanadamu
kwani hiki ndicho kipindi cha harakati na joto la maisha. Hiki ndicho
kipindi cha mvuto na matamanio, kijana anaupenda ulimwengu nao unampenda.
Ni kipindi ambacho kijana anakuwa katika mtihani mkubwa wa kuyashinda
majaribu na matamanio ya kimwili na kimali. Akifaulu kuvuka katika kipindi
hiki ndio kafaulu katika maisha yote. Ujana ni kipindi cha mpito cha
nguvu/harakati kilicho baina ya vipindi viwili vya udhaifu. Kipindi cha
utoto, kipindi cha kutojiweza na kipindi cha utu uzima (ukongwe), kipindi
tegemezi. Qur-ani Tukufu inavielezea vipindi hivi,tuitegee sikio: “ALLAH
NDIYE ALIYEKUUMBENI KATIKA UDHAIFU (wa tumboni kwa mama na utoto baada ya
kuzaliwa) NA BAADA YA UDHAIFU (huo) AKAFANYA NGUVU (za ujana), KISHA BAADA
YA NGUVU (hizo) AKAUFANYA UDHAIFU NA UZEE…” [30:54]
|