|
Wapenzi wasomaji wetu.
Assalaamu Alaykum Warahmatullah!
Ni baada ya siku chache tu kwa msaada wake Allah Karim
utakuwa unapumua na kuishi ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Mwezi
ambao huwapa waislamu fursa ya kuitekeleza mojawapo ya nguzo tano za
Uislamu, swaumu ya Ramadhani. Katika kuuheshimu, kuutukuza na kuuenzi
mwezi huu mtukufu, Mtumishi wa uma {WEBSITE UISLAMU}, itakutumikia kwa
kukuletea mfululizo wa makala maalumu zihusianazo na mwezi wako huu. Lengo
kuu la makala hizi likiwa ni kukumbusha wewe msomaji wetu:-
Utukufu wa mwezi wa Ramadhani ili uuthamini, kwani
asiyekujua hakuthamini.
Swaumu ya Ramadhani na yote yanayofungamana nayo, ili
uweze kufunga kama alivyoamrisha Allah na Mtume wake.
Haya ndiyo malengo mama ya makala hizi ambazo tunatumai
kwa msaada na taufiq yake Allah yatakunufaisha na kujibu maswali yako
mengi. Ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yanakutatiza kuhusiana
na swaumu hii ya Ramadhani.
Naam, Ramadhani hiyo mlangoni mwako inabisha hodi. Wewe
kama muislamu umejiandaje kuupokea mwezi wako huu mtukufu? Je, wewe ni
mmoja wa wale wanaoupokea mwezi wa Ramadhani kwa kile kinachojulikana kama
VUNJA JUNGU?
Hebu na tujiulize kwa pamoja, tulivunjao hilo jungu mwaka
hata mwaka na wale tusiolivunja, vunja jungu ni nini khasa? Bila ya shaka
mtakubaliana nasi kwamba vunja jungu kama litafsirikanavyo kutokana na
matendo yatendwayo na wavunja jungu katika kulivunja kwao hilo jungu. Ni
mkono wa kwaheri unaopungwa kwa maasi mbalimbali kwa ajili ya kuingia kwa
mwezi mtukufu wa Ramadhani. Wavunja jungu huitumia fursa ya zile siku
mbili tatu kabla ya kuandama kwa mwezi mwandamo unaoashiria kuanza kwa
funga tukufu ya Ramadhani. Kuogelea na kupiga mbizi maradufu katika maasi
waliyokuwa wakiishi nayo katika kipindi cha ile miezi kumi na moja nje ya
Ramadhani. Kwa hivyo basi, vunja jungu kwa mlevi ni kulewa sana kwani
hataipata fursa hiyo tena ila baada ya kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani.
Vunja jungu kwa mzinifu ni kuzini sana na kutengana na kimada wake
kuipisha Ramadhani, kisha mchezo uendelee baada ya Ramadhani. Vunja jungu
kwa mpenzi wa muziki ni kukesha katika kumbi za starehe akicheza na kunywa
kufidia ile fursa atakayoikosa kwa sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu.
Mbele za watu hawa Ramadhani ni mithili ya gereza/kifungo kinachowaondolea
na kuwanyang`anya uhuru wa kuishi kama wapendavyo kwa kufuata matashi na
matamanio ya nafsi zao. Hawa wanasahau kwamba wanawajibika kuishi kwa
mujibu wa muongozo wa Mola Muumba wao na sio kwa kuongozwa na matashi yao!
Kwa ujumla vunja jungu ni kushindana katika aina mbalimbali za maasi kwa
sababu ya kuingia kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao hautoi uwanja wa
maasi hayo kwa mijibu wa fikra zao potofu. Kwa nini tunasema kwa mujibu wa
fikra zao potofu, hilo linatokana na ukweli kwamba hakuna kibali wala
uhalali wa kufanya maasi na mtu kuishi kama apendavyo nje ya Ramadhani.
Ikiwa vunja jungu linaashiria jambo, basi jambo hilo
halitakuwa jingine zaidi ya kuonyesha kufilisika kiimani kwa huyo mvunja
jungu. Kwani muumini wa kweli hawezi kuvunja jungu, kwa kuwa anatambua
kwamba kufanya hivyo ni kumuasi Allah Mola Muumba wake. Kwa muumini wa
kweli kujiepusha na maasi na kumtii Mola wake ni zoezi linaloyatawala
maisha yake yote. Bila ya kuangalia kuwa huu ni mwezi wa Ramadhani au ni
nje ya Ramadhani. Kuagana na maasi eti kwa sababu tu ya kuingia kwa mwezi
mtukufu wa Ramadhani, kisha kuyarejea tena baada ya kumalizika kwake. Huo
tukubali au tukatae ni UDHAIFU WA IMANI na si vinginevyo. Kwani huyo Mola
wa Ramadhani unayeacha maasi ndani yake kwa ajili yake, ndiye Mola wa hiyo
miezi mingine unayojihalalishia maasi ndani yake. Amri ya kumtii Mola wako
kwa kuyatekeleza yote aliyokuamrisha na kuyaacha yote aliyokukataza
inauhusu mwezi wa Ramadhani na baki ya miezi mingine isiyo Ramadhani.
Kumuabudu Mola wako ndani ya Ramadhani tu ni kujiuundia utaratibu wa ibada
kinyume na ule aliokupangia Allah Mola Muumba wako. Elewa kufanya kwako
hivi ni sawa na kusema kuwa utaratibu wa ibada aliokuwekea Mola wako aliye
mjuzi wa manufaa na maslahi yako ama haufai au umepitwa na wakati. Na
kwamba wewe kama kiumbe unaweza kujiundia utaratibu utakaokudhaminia
manufaa na mafanikio katika ulimwengu wako huu na ule ujao. Elewa kwa
mtindo na mtaji wako huo siku ya kiyama Allah atakuambia ujilipe wewe
mwenyewe kwa kuwa yeye hakukuamrisha kufanya ibada kwa utaratibu huu
unaokwenda nao sasa.
Ewe ndugu mpenzi wee! Elewa na ufahamu fika kwamba
Ramadhani ipokelewayo na kukaribishwa na vunja jungu haitakuwa na athari
yo yote kwako wewe ambaye ndiwe mlengwa wa Ramadhani na wala sio Mola wako.
Kwako Ramadhani haitakuwa ila mithili ya kujenga nyumba angani bila ya
kuwa na msingi imara uliokita ardhini. Ewe ndugu mpenzi mvunja jungu,
utaendelea kulivunja hilo jungu na kumuasi Mola wako mpaka lini?! Hebu
jiulize, nini utakuwa mwisho wa huku kuvunja jungu kwako?! Tangu umeanza
kuvunja jungu na bila shaka ni jungu la maasi umepata na kuvuna nini?!
Ndugu mpenzi hebu ihurumie nafsi yako kwa kuitegea sikio la usikivu kauli
hii tukufu ya Mola wako: “ANAYEFANYA MEMA ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI
YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (ya nafsi) YAKE (vile vile)…”
[41:46]
Aya inakuongoza kutambua kwamba unapovunja jungu, hufanyi
hivyo ila ni kwa hilaki na maangamivu ya nafsi yako wewe mwenyewe leo hapa
duniani na kesho kule akhera. Ambapo utapewa daftari la amali zako uikute
na vunja jungu yako, hapo ndipo utasema: “…OLE WETU! NAMNA GANI
MADAFTARI HAYA! HAYALIACHI DOGO WALA KUBWA ILA YAMELIDHIBITI (yameliandika)!
NA WATAKUTA YOTE YALE WALIYOYAFANYA YAMEHUDHURIA HAPO; NA MOLA WAKO
HAMDHULUMU YO YOTE”. [18:49]
Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Jibril
alinijia na akaniambia: Ewe Muhammad! Ishi utakavyoishi, hakika wewe ni
mwenye kufa. Na penda ukipendacho hakika utatengana nacho, na tenda
ulitakalo hakika utalipwa kwalo…” Al-Baihaqiy
Elewa ewe ndugu mpenzi ukiwa mwana kuelewa, elewa kwamba
kwa mujibu wa hadithi hii:-
Vunja jungu yako ina mwisho wake ambao ni kufa
kunakoashiria mwanzo wa safari ngumu ya kuhudhurishwa mbele ya Mola wako.
Hii ndiyo siku anayoitaja Mola wako kwa kauli yake tukufu: “NA IOGOPENI
SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA
UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO HAWATADHULUMIWA”. [2:281]
Lewa sana kwani pesa ni zako,zini sana na endelea kuvunja
jungu, lakini tambua kuwa iko siku moja utalipwa kwa yote uliyoyatenda
hapa duniani: “BASI ANAYEFANYA WEMA (hata) WA KIASI CHA UZITO WA MDUDU
CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE. NA ANAYEFANYA UOVU (hata) WA KIASI CHA UZITO WA
MDUDU CHUNGU ATAONA JAZAA YAKE”. [99:7-8]
Ewe mvunja jungu wee! Hebu waidhika na sehemu hii ya kauli
ya swahaba wa Mtume;Sayyidna Abdullah Ibn Abbas-Allah amuwiye radhi:
“Ewe mtenda dhambi wee! Usijiaminishe na matokeo ya dhambi yako na
tambua kwamba kiifuatiacho dhambi hiyo ni kikubwa kuliko dhambi yenyewe.
Kwani kule kutokuwaonea kwako haya malaika walioko kuliani
na kushotoni kwako wakati unapofanya dhambi, hakupungui kuwa ni dhambi.
Na kicheko chako wakati unatenda dhambi na ilhali hujui
Allah atakufanya nini, ni kikubwa zaidi kuliko hiyo dhambi uitendayo.
Na kuichelea kwako dhambi unapofanikiwa kuitenda, ni
kukubwa zaidi kuliko hiyo dhambi yenyewe.
Na kuihuzunikia kwako dhambi kwa kushindwa kuitenda, ni
kukubwa zaidi kuliko dhambi husika.
Haya mpenzi mvunja jungu, ikiwa mpaka hapa bado
hujawaaidhika na ukaacha kulivunja hilo jungu, hebu zidi kutega sikio:
Mtu mmoja alimwambia Sufyaan Thauriy-Allah amuwiye
radhi-nipe nasaha ambazo nikizifanyia kazi sitathubutu kumuasi Allah.
Sufyaan akamwambia: Yakumbuke mambo matano:
Je, inastahiki kwako kumuasi Allah na ilhali yeye ndiye
anayekuruzuku?
Je, unadhani kuwa wewe unamuasi Allah na ilhali yeye
anakuona?
Je, unaweza kumuasi Allah nje ya ufalme/milki yake?
Je, unaweza kuyaakhirisha mauti yakikujia?
Je, siku ya kiyama utakuwa una uwezo wa kujiondoshea
adhabu?
Yule mtu akajibu: Siwezi lo lote katika hayo. Sufyaan
akamwambia: Basi vipi unathubutu kumuasi yule anayekuruzuku, anakuona,
nawe uko katika milki yake, akakuandikia mauti na wala huwezi kuizuia
adhabu yake isikufike? Akasema mtu yule: Wallah sitamuasi muda wa uhai
wangu.
Hebu nawe mvunja jungu, jiulize maswali matano hayo halafu
ndio uamue ama kulivunja jungu au kutokulivunja. Kumbuka ewe ndugu
muislamu kwamba:-
Kuvunja jungu ni kumuasi Allah na Mtume wake: “NA
ANAYEMUASI ALLAH NA MTUME WAKE, NA KUIRUKA MIPAKA YAKE (Allah) ATAMUINGIZA
MOTONI. HUMO ATAKAA MILELE NA ATAPATA ADHABU ZIFEDHEHESHAZO”. [4:14]
Kuvunja jungu ni kuudhihaki mwezi mtukufu wa Ramadhani. Na
kuudhihaki mwezi huu hakumaanishi kingine zaidi ya kuidhihaki Qur-ani
Tukufu. Nako huku kuidhihaki Qur-ani, hakika si vinginevyo ila ni
kumdhihaki aliyeshushiwa Qur-ani Mtume. Na hakuna anayethubutu kupinga
kwamba kumdhihaki Bwana Mtume ni kumdhihaki Allah akiyemtuma. Na huko
kumdhihaki Allah ni ukafiri tu na si vinginevyo: “AMA WALE WALIOKUFURU,
NITAWAADHIBU ADHABU KALI KATIKA DUNIA NA AKHERA, WALA HAWATAPATA WASAIDIZI
WA KUWASAIDIA”. [3:56]
Vunja jungu ni khadaa na ghururi za dunia. Uovu basi si
huko kukhadaika, bali ni kushikilia kukhadaika baada ya kutanabahishwa.
Mwisho Mtumishi wa uma {WEBSITE UISLAMU} anakutakieni kila
la kheri, fanaka na baraka tele za Allah katika mwezi huu wa Ramadhani.
Allah Karim tunamuomba aijaalie Ramadhani hii kuwa ni yenye kuleta
mabadiliko na mapinduzi ya kiimani katika nyoyo za waislamu po pote pale
walipo ulimwenguni.
Wasalaamu Alaykum Warahmatullah.
Shahrun Mubaaraku.
|