|
KALIMA YA
EIDIL-FITRI (WAADHI WA EID).
Ndugu waislamu,
Assalaamu Alaykum!
Himda njema zote
zinamstahikia Allah na rehema na amani zimuendee Nabii Muhammad, maswahaba
na aali zake wote na kila awafuataye kwa wema mpaka siku ya Kiyama.
Ama baad,
Ndugu zanguni
waislamu! Sote tunakubaliana kwamba siku ya Eid ni siku ya furaha, na ni
siku ambayo mmehalalishiwa kula na kunywa mchana. Ni siku inayoashiria
kumalizika kwa ibada tukufu na kongwe ya swaumu ya Ramadhani. Ni siku ya
watu kuvaa vizuri, kutembeleana, kusaidiana na kuwalisha watu chakula.
Hebu itegee sikio pamoja nami kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani
zimshukie: “Inapokuwa siku ya Eidil-Fitri, malaika hukaa mwanzoni mwa
njia wakalingana: Damkeni enyi waislamu, enendeni kwa Mola Mkarimu
aneemeshaye kisha kulipa thawabu juu ya neema hizo. Mmeamrishwa kusimama
usiku kuswali (taraweh) mkasimama na mliamrishwa kufunga mchana mkafunga.
Na mkamtii Mola wenu, pokeeni zawadi zenu. Eeh hakika Mola wenu amekwisha
kusameheni, basi rejeeni majumbani mwenu hali ya kuwa mmeongoka. Nayo ni
siku ya zawadi na siku hii huitwa mbinguni (siku ya zawadi)”.
Twabaraaniy
Siku ya Eid ni siku
ya mahafali. Waislamu wamehitimu mafunzo yao ya mwezi mmoja katika Chuo
Kikuu Cha Ucha-Mungu (swaumu). Leo ndio siku ya kutunukiwa na kukabidhiwa
wahitimu vyeti vyao. Na leo ndio kila mtu atajua matokeo ya mafunzo yake
kama amefaulu au amefeli. Hili litajulikana kutokana na namna
atakavyoisherehekea siku yake hii ya leo.
Ndugu zanguni
wapenzi! Katika kumalizika mwezi mtukufu wa Ramadhani tunapata fundisho
moja kubwa sana. Nalo ni kwamba kama vile tulivyoushuhudia mwanzo wa mwezi
wa Ramadhani na leo hii tunashuhudia kumalizika kwake. Tujiulize na
tutafakari hili linaashiria nini katika maisha yetu ya kila siku? Ikiwa
hili linatoa ishara ya kitu/jambo, basi jambo hilo litakuwa si jingine.
Bali ni kwamba tujue kwa yakini kuwa kila chenye mwanzo hakina budi kuwa
na mwisho. Isipokuwa Allah pekee yeye ndiye asiye na mwanzo wala mwisho.
Tuukiri na kuukubali ukweli huu usiopingika, tujue na tufahamu kuwa kama
ambavyo kila mmoja wetu alikuwa na siku ya kuja kwake katika ulimwengu
huu. Kadhalika anayo siku inayomngojea ya kuondoka kutoka katika ulimwengu
huu umalizikao kuyaendea ima maisha ya milele peponi au motoni. Tusome na
tuzingatie: “KILA KILICHO JUU YAKE (ardhi na mbingu) KITATOWEKA
(kitaondoka). INABAKI DHATI YA MOLA WAKO (tu mwenyewe) MWENYE UTUKUFU NA
HISHIMA”.
[55:26-27]
Ndugu zanguni,
tujiandae vema na mapema na siku hii ngumu na nzito ambayo haikwepeki,
hatuna budi tutakutana nayo tu. Siku hii ndio mwanzo wa safari ya
kuhudhurishwa mbele ya mahakama yenye kila aina ya uadilifu, haki na
usawa. Kwa ajili ya kuhesabiwa na kulipwa kwa mujibu wa amali zetu
tulizozitenda hapa duniani bila ya kudhulumiwa mtu. Kitakachofuatia baada
ya hapo ni: “...KUNDI MOJA LITAKUWA PEPONI NA KUNDI JINGINE MOTONI”.
[42:7]
Kuwa katika kundi la
peponi/motoni, huo ni uchaguzi wako mwenyewe na hili litategemea jinsi
utakavyo zichanga karata za maisha yako katika ulimwengu huu wa mpito.
Utavuna pepo/moto kwa akili, nguvu na mali yako mwenyewe. Tuiogopeni ndugu
zanguni siku hii: “NA IOGOPENI SIKU AMBAYO MTARUDISHWA KWA ALLAH, KISHA
VIUMBE WOTE WATALIPWA KWA UKAMILIFU YOTE WALIYOYACHUMA; NAO
HAWATADHULUMIWA”. [2:281]
Naam, mwezi wa
Ramadhani umemalizika na bila ya shaka utatushuhudia mbele ya Allah kwa
yote mema/mabaya tuliyoyatenda ndani yake. Katika mwezi huu mtukufu sote
tumeshuhudia jinsi misikiti ilivyokuwa ikijaa waumini katika swala zote za
fardhi, hata ile swala nzito na ngumu ya alfajiri. Misikiti ilikuwa
ikiamirishwa kwa kusomwa sana Qur-ani Tukufu na kudhukuriwa sana Allah.
Takriban wakati wote usiku na mchana utawakuta waumini misikitini
wakifanya namna kwa namna za ibada. Na utaviona vikundi vya ilimu, waumini
wanasomeshana, kukumbushana na kupeana nasaha kuhusiana na dini yao. Yote
haya tumeyaona na kuyashuhudia ndani ya mwezi wa Ramadhani, lakini kwa
masikitiko makubwa leo mwezi umemalizika na mambo yake yote mema na mazuri
yanamalizika pamoja nao. Hutayaona tena hadi Ramadhani ya mwakani panapo
uhai na majaliwa. Ni kweli kuwa Ramadhani imekwisha, lakini yule
tuliyekuwa tunafunga na kuswali kwa ajili yake yu hai milele, hamaliziki
na wala haishi kama ilivyokwisha Ramadhani. Kwa hivyo ni wajibu wetu
kuendelea kuuelekeza utii wetu kwake hata nje ya Ramadhani kama
tulivyokuwa tukifanya ndani ya Ramadhani. Eh! Hasara, msiba na majuto
yaliyoje kwa waja hawa, kama kwamba walikuwa wanauabudu mwezi wa Ramadhani
na sio Mola wa mwezi wa Ramadhani! Mwezi ukiisha, hakuna tena kuswali,
kufunga, kusoma Qur-ani, wala..., wala....Hii ni dalili na ishara ya wazi
ya kutokukubaliwa kwa swaumu na amali zao nyingine walizozitenda ndani ya
mwezi wa Ramadhani. Kwani amali ya mja ikikubaliwa na kupokelewa, Mola
humzidishia mja huyo taufiki na kutengenea. Hapo ndipo utamuona kila siku
anazidi na kuendelea kumtii Mola wake.
Ndugu zanguni
waislamu, ni muhali kabisa kwa mtu aliyefunga kwa Ikhlaaswi, halafu akawa
leo baada ya swala ya Eid ndio anaagana na msikiti. Haswali tena hadi
Ramadhani ya mwakani ambayo hana dhamana nayo. Ikiwa itakuwa hivi ni wazi
kuwa swaumu ya mja huyu haikumfikisha kwenye lengo lake ambalo ni
kumuandaa na kumfinyanga mja kuwa mcha-Mungu. Tusome na tuzingatie:
“ENYI MLIOAMINI! MMELAZIMISHWA KUFUNGA (swaumu) KAMA WALIVYO LAZIMISHWA
WALIOKUWA KABLA YENU ILI MPATE KUMCHA ALLAH”. [2:183]
Ni ukweli
usiopingika kwamba mtu hawezi kuwa mcha-Mungu bila ya kushikamana na swala
tano. Ndugu zanguni, Allah aliwaamrisha malaika pamoja na Ibilisi ambaye
alikuwemo kundini kumsujudia Nabii Adam-Amani ya Allah imshukie.
Wamsujudie hali ya kumuamkia na wala sio kwa njia ya kumuabudu. Iblisi kwa
ushupavu na upasito aliokuwa nao alikataa kuitekeleza amri hii ya Mola
wake. Ni kwa sababu hii ya kuikhalifu na kukataa kuitii amri hii, Allah
akamfukuza na kumtoa Iblisi huko alikokuwa kwenye neema za daima. Na
akamtenga mbali na rehema zake (akamlaani) na isitoshe kesho akhera
ataingia motoni ikiwa ni jazaa ya inadi na kibri chake. Basi wewe ndugu
yangu mpenzi usiotaka kuswali, hivi hujioni kuwa wewe ni mbaya zaidi
kuliko Iblisi? Pengine utajiuliza kwa nini au utaona kuwa unatukanwa kwa
kufananishwa na kiumbe mbaya huyu aliyelaaniwa! Lakini huo ndio ukweli na
utaendelea kuwa ndio ukweli maadam wewe ni tariku-swala (mwenye kuacha
swala). Hakuna cha kuubadilisha ukweli huu ila ni wewe kuwa miongoni mwa
wenye kuswali kama alivyoamrisha Allah Mola Muumba wako. Naam, hii ni kwa
sababu Iblisi alikataa kumsujudia baba yetu Nabii Adam sijida ya maamkizi
kwa amri ya Allah. Wewe usioswali leo, unakataa kumsujudia sijida ya ibada
yule aliyemuumba Nabii Adam. Iblisi alikataa kusujudu mara moja tu katika
umri wake wote, wewe usioswali unakataa kusujudu mara thelathini na nne
(34) kila siku. Naam ,mara 34 kwa siku, kwani jumla ya rakaa za swala tano
za fardhi ulizofaradhishiwa na Allah kuziswali kila siku ni rakaa kumi na
saba. Mbili alfajiri, adhuhuri nne, laasiri nne, maghribi tatu na Ishaa
nne, jumla ni rakaa kumi na saba. Na kila rakaa moja ina jumla ya sijida
mbili, ukizidisha kumi na saba kwa mbili utapata jumla ya sijida
thelathini na nne (34), hizo ndizo sijida unazopaswa kumsujudia Mola wako
kila siku. Hebu iangalie tena adhabu aliyopewa Iblisi kwa kuacha sijida
moja tu, hii inamaanisha kuwa mwenye kuacha sijida 34 kila siku anastahiki
kupata adhabu kali zaidi kuliko aliyopewa Iblisi. Sikwambii tena asoswali
wiki, mwezi, mwaka, muongo (decade) au umri mzima anastahiki adhabu gani.
Eeh! Ndugu yangu, kiumbe dhaifu wee! Ionee huruma nafsi yako, acha ukaidi
utakaokuletea majuto, huiwezi tena huiwezi hata chembe adhabu ya Mola
wako. Badili mwenendo wako sasa kabla hujachelewa, tusome na tuzingatie:
“...NA BILA SHAKA ADHABU YA AKHERA NI KALI ZAIDI NA IENDELEAYO SANA”.
[20:127]
Pia kuna khatari
kubwa ya kuwa kafiri mtu asoswali, hebu itegee sikio kauli hii ya Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “YE YOTE atakayeacha swala kwa
makusudi, bila shaka atakuwa AMEKUFURU”.
Ndugu zanguni
waislamu, inasikitisha sana jinsi waislamu tunavyoisherehekea sikukuu yetu
hii. Siku ya Eid ndiyo siku ambayo waislamu wenyewe wanautukanisha uislamu
wao na kuudhihirishia ulimwengu kwamba akthari ya wafanyao maasi ni
waislamu. Mtu alikuwa hawezi kukesha msikitini kufanya ibada, siku ya leo
atakesha katika ulevi, atakunywa hadi atajimwagia. Huyu eti anasherehekea
kumalizika kwa mfungo mtukufu wa Ramadhani. Sub-haanalla! Na huyu si
mwingine bali ni yule yule muislamu tuliyekuwa naye msikitini katika
kipindi chote cha Ramadhani akiswali na kufunga pamoja na sisi. Huyu
haisherehekei Eid bali ukweli na uhalisia wa mambo ni kwamba
anausherehekea moto wa Jahanamu unaomngojea iwapo hataidiriki toba kabla
ya kufikwa na mauti. Na huyu ndiye mtu aliyefeli vibaya kabisa katika
mafunzo ya Chuo Kikuu Cha Ucha-Mungu (swaumu). Siku ya Eid ndio siku
ambayo utawaona dada zetu wamevaa mavazi ya ajabu ajabu na kuwa kama mbuzi
wasio na mchunga, wanauuza utu wao na kununua maradhi sambamba na moto wa
milele. Ili muradi siku ya Eid, watu watashindana katika kumuasi Mola wao
na kumfurahisha shetani. Wote hawa tunawaasa na kauli hii tukufu ya Allah:
“AMA YULE ALIYEASI. NA AKAPENDA ZAIDI (akayafadhilisha maisha) YA DUNIA.
BASI KWA HAKIKA JAHANAMU NDIYO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE. NA AMA YULE
ALIYEOGOPA KUSIMAMISHWA MBELE YA MOLA WAKE, AKAIKATAZA NAFSI YAKE NA
MATAMANIO (maovu). BASI (huyo) PEPO NDIO ITAKAYOKUWA MAKAZI YAKE”.
[79:37-41]
Ndugu zanguni
waislamu, funga ya Ramadhani imemalizika, LAKINI hii haimaanishi kuwa
muislamu hana tena fursa ya kufunga hadi Ramadhani ya mwakani. La hasha,
bali anayo fursa adhimu ya kujikurubisha na kujipendekeza zaidi kwa Mola
wake kwa kufunga swaumu mbali mbali za suna. Miongoni mwa swaumu hizo za
suna ni kufunga siku sita za mfunguo mosi (Shawwal). Imepokelewa hadithi
na Abuu Ayuub-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani
zimshuie-amesema: “Atakayeufunga mwezi wa Ramadhani, halafu
akaufuatishia na siku sita za mfunguo mosi. Itakuwa ni kama kufunga mwaka
mzima”.
Muslim
Ndugu zanguni hayo
ndio malipo na ujira adhimu na mnono wa funga ya Ramadhani iambatanishwayo
na funga ya siku sita za mfunguo mosi. Tumeweza kufunga mwezi mzima, hivi
ni kweli tutashindwa kufunga siku sita! Ikiwa tuna nia ya kujipendekeza na
kujikurubisha kwa Mola wetu kwa maslahi na manufaa yetu wenyewe
hatutashindwa. Haya na tujihimize ndugu zanguni, kwani: “ANAYEFANYA WEMA
ANAJIFANYIA (mwenyewe) NAFSI YAKE, NA MWENYE KUTENDA UBAYA NI JUU (nafsi)
YAKE (vile vile); NA MOLA WAKO SI DHALIMU (hata kidogo) KWA WAJA
(wake)”. [41:46]
“...NA KHERI YO
YOTE MNAYOITANGULIZA KWA AJILI YA NAFSI ZENU MTAIKUTA KWA ALLAH IMEKUWA
BORA ZAIDI NA INA THAWABU KUBWA SANA...” [73:20]
Mwisho, Website yenu
WEBSITE UISLAMU inakutakieni waislamu wote po pote mlipo ulimwenguni kote
kheri, baraka, amani, furaha na radhi ya Allah katika sikukuu hii ya
Eidil-Fitri. Tunawapongezeni nyote kwa kusema: TAQABBALAL-LAAHU MINNAA WA
MINKUM WA AHYAAKUM. KULLU AAMUN WA ANTUM BIKHAYRI!
Wasalaamu Alaykum
Warahmatullaah Wabarakaatuh!
|