Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MINBARI YA RAMADHANI-

SWALA YA TARAWEHE

Faida

 

    9.        Kushikamana na kitendo cha Sayyidna Umar, ndio kushikamana na Sunna ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie:

         Tunaharakia kusema na tunawaambia maimamu wa Ijitihadi katika zama hizi: Hakika aliyo yafanya Umar au aliyo yaamrisha Umar, si uzuzi (bidaa) katika dini. Bali hilo ni kushikamana na muongozo wa Mtume na ni kuifuata Sunna ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-kwa sababu zifuatazo:

                (a)          Kwamba Sayyidna Umar Bin Al-Khatwaab, alipewa na Mtume jina la “Al-Faarouq”, kwa sababu Allah aliifarikisha (aliitenganisha) haki na batili kupitia kwake. Na alitenganisha kwaye uwongofu na upotofu, basi yeye ni Al-Faarouq Umar-Allah amuwiye radhi.

               (b)          Yeye ni mletewa ilhamu (ufahamu) ambaye hasemi ila ambalo ndani yake imo haki na ilivyo ndivyo, na kheri (wema) na uongozi, kwa sababu ya nuru ya uoni (utambuzi) wake. Na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema juu yake: “Hakika Allah Atukukiaye, ameiweka haki kwenye ulimi na moyo wa Umar”. Tirmidhiy & JAAMIUL-USWUUL 08/608. Na amesema: “Hakika walikuwemo miongoni mwa wa kabla yenu wapewa ilhaamu, basi kama yuko yeyote katika umati wangu, basi bila ya shaka huyo ni Umar”. Bukhaariy [07/40]-Allah amrehemu.

                (c)          Qur-ani imeshuka mahala pengi ikiwafikiana na rai/maoni ya Umar. Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Umar Bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye amesema: “Nimewafikiana na Mola wangu katika sehemu tatu: katika Maqaamu Ibraahim, katika suala la Hijaabu na katika kadhia ya mateka wa Badri. Mimi nilisema: Ewe Mtume wa Allah! Unaonaje lau tungepafanya Maqaamu Ibraahim kuwa ni mahala pa kuswalia? Ikashuka aya “...NA ALIPO KUWA AKISIMAMA IBRAHIM PAFANYENI PAWE PA KUSWALIA...” [02:125] Na nilisema: Ewe Mtume wa Allah! Hakika wanaingia kwa wake zako, wema na waovu, basi unaonaje lau utawaamrisha wavae Hijaabu? Hapo ikashuka aya ya Hijaabu “... NA MNAPO WAULIZA WAKEZE HAJA WAULIZENI NYUMA YA MAPAZIA...” [33:53] Na wake za Mtume-Rehema na Amani zimshukie-walikusanyika juu yake katika wivu, nikasema: “Asaa Mola wake Mlezi, akikupeni talaka, akampa wengine badala yenu nyinyi, walio bora kuliko nyinyi”. Ikashuka aya kama hivyo”. Bukhaariy-Allah amrehemu.

Basi ikiwa Qur-ani inashuka ikimuwafiki/ikikubaliana na rai ya Umar, ni vipi basi maswahaba wasiitwae kauli yake na wakakongamana juu yake?!

Na Imamu Tirmdhiy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Abdullah Bin Umar-Allah awawiye radhi-kwamba yeye amesema: “Halikupata katu kuwashukia watu jambo, wakalizungumza na akalizungumza Ibn Al-Khatwaab, ila ilishuka Qur-ani katika jambo hilo kwa namna alivyo sema Umar”. Tirmdhiy & JAAMIUL-USWUUL 08/608.

               (d)          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliwaamrisha Waislamu kushikamana na muongozo wa makhalifa waongofu na Sunna ya Abubakar na Umar. Akasema: “Na hakika atakaye kuwa na maisha marefu miongoni mwenu, basi ataona ikhtilafu nyingi. Basi (wakati huo), nyinyi shikamaneni na Sunna (mwendo) wangu na Sunna ya makhalifa waongofu, viongozi wenye kuongoza. Ziumeni kwa magego”. Abu Daawoud & Tirmidhiy-Allah awarehemu.

Na amesema Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Wafuateni wale baada yangu, Abubakar na Umar”.

Na amesema Abdullah Bin Masoud-Allah amuwiye radhi: “Yeyote mwenye kuwa mshika Sunna, basi na ashikamane (afuate) na Sunna ya walio kwisha kufa, kwa sababu aliye hai haiaminiwi juu yake fitina. Hao (walio kufa) ni maswahaba wa Muhammad-Rehema na Amani zimshukie-walikuwa ni wabora wa umma huu. Wema wao kwa nyoyo, wenda kina wao kwa elimu na wachache wao kwa taklifu. Allah aliwachagua kusuhubiana na Mtume wake na kuisimamisha dini yake. Basi ukirini ubora wao na zifuateni nyoyo zao na shikamaneni na mnacho kiweza katika tabia na mwendo wao. Kwani wao walikuwa juu ya uwongofu nyoofu”. Ibn Abdul-Barri [JAAMIU BAYAANIL-ILMI WAFADHWLIHI 02/97].

 

Mimi ninasema: Basi je, ni nani anaye stahiki zaidi kufuatwa uwongofu (muongozo) wake kuliko Abubakar na Umar?! Na ni vipi kuwe kumfuata Umar katika lile alilo washariia Waislamu ni “Bidaa potofu”, kama wanavyo sema baadhi ya watu majahili miongoni mwa wanao dai kuwa na elimu?!

Amesema Ibn Al-Athiyr-Allah awarehemu-katika kuizungumzia hadithi iliyo pokewa kutoka kwa Bukhaariy-Allah amrehemu-kutoka kwa Umar katika kauli yake: “Bora ya bidaa, ni hii”. Amesema maneno ambayo nassi (nukuu) yake ni: “Neno bidaa linatokana na neno Ibtidaa – (kuanzisha upya/kuzua/kuleta kisicho kuwepo kabla). Na hiyo Ibtidaa (kuzua) ikiwa kinyume na aliyo amrisha Allah na Mtume wake, basi huko kuko katika wigo wa kulaumiwa na kukanushwa. Na kukiwa kunatuka (kunaingia) chini ya uenevu wa aliyo yapendezesha Allah na akayahimiza au Mtume wake, basi hicho kiko kwenye wigo wa kusifiwa. Kama aina ya wema na ukarimu na kutenda mema. Basi hii (Ibtidaa) ni katika amali (matendo) zenye kusifiwa na inatiwa nguvu na hadithi “Atakaye anzisha Sunna (mwendo) njema, atapata ujira wake (hiyo Sunna) na ujira wa atakaye itendea kazi”. Na hilo linaungwa mkono na kauli ya Sayyidna Umar Bin Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-katika swala ya Tarawehe: “Bora ya bidaa, ni hii”. Kwa kuwa lilikuwa katika matendo ya kheri na linaingia katika wigo wa kusifiwa, akaliita bidaa na akalisifia. Na hiyo (swala) ajapo kuwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliiswali, ila yeye aliiacha, hakuidumisha na wala hakuwakusanya watu juu yake. Basi kule kuidumisha kwake Umar (swala hiyo) na kuwakusanya watu juu yake na kuwapendezeshea, ni bidaa. Lakini hiyo ni bidaa njema, yenye kusifiwa”. [JAAMIUL-USWUUL 01/281]

Na hakika si vinginevyo, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliikata swala ya Tarawehe, kwa ajili ya kuuonea huruma umati wake. Na Sayyidna Umar-Allah amuwiye radhi-akawa miongoni mwa walio wazindua watu juu yake (Sunna hii) na akaisunisha kwa udaima (miaka yote). Basi kwa ajili hii, yuna yeye ujira wake na ujira wa wenye kuitendea amali mpaka siku ya Kiyama. [JAAMIUL-USWUUL 06/123]

Na amesema Ibn Hajar Al-Asqalaaniy katika FAT-HUL-BAARIY: Na asili ya bidaa, ni lile lililo zushwa bila ya kuwa na mfano tangulizi, na hutumika (neno hili) katika sheria kwenye mkabala wa Sunna, na hapo huwa ni lenye kutaiwa (kulaumiwa na kusemwa vibaya). Na uthibitifu ni kwamba hiyo (bidaa) ikiwa ni miongoni mwa yanayo bimbirikia chini ya lenye kuonwa zuri katika Sharia, basi nalo hilo huwa zuri, kama alivyo sema Umar: “Bora ya bidaa, ni hii”. Na ikiwa ni miongoni mwa yanayo bimbirikia chini ya yenye kuonwa vibaya katika Sharia, basi hilo nalo huwa baya. Na kama si hivyo, basi hilo ni katika fungu la Mubaaha”. [FAT-HUL-BAARIY, SHEREHE YA BUKHAARIY, 04/253]

Kisha akaendelea kusema-Allah amrehemu: Na kisimamo cha Ramadhani ni Sunna, kwa sababu Umar hakika si vinginevyo, alikichukua kutoka kwenye kitendo cha Mtume-Rehema na Amani zimshukie. Na hakika si vinginevyo, Mtume alikiacha kwa kuchelea kisije kufaradhishwa na Mtume alipo kufa, hofu hiyo ikawa imeondoka. Kukawa na nguvu mbele za Umar kuwakusanya watu nyuma ya Imamu mmoja, kwa sababu ya utengano wa neno unao patikana ndani ya kukhitilafiana. Na kwa sababu ya kukusanyika nyuma ya Imamu mmoja kunawatia uchangamfu waswaliji wengi... Na wala haikutuka katika riwaya hii (ya Bukhaariy) idadi ya rakaa ambazo alikuwa Ubayyi Bin Ka’ab akiwaswalisha. Na pamekindanwa katika hilo, pakasemwa: Hakika hizo ni rakaa kumi na moja, na walikuwa wakisoma aya mia mbili na wakitegemea vifimbo kutokana na urefu wa kisomo. Na pamesemwa: Ni rakaa kumi na tatu. Na Imamu Maalik-Allah amrehemu-amepokea kwa njia ya Yazid Bin Khuswaifah: Kwamba hizo ni rakaa ishirini, na (idadi) hii inachukuliwa bila ya (kuchanganya na) Witri.

Na imepokewa kutoka kwa Yazid Bin Roumaan: “Watu walikuwa wakisimama katika zama za Umar kwa rakaa ishirini na tatu”.

Na amesema Atwaau: “Niliwadiriki katika Ramadhani wakiswali rakaa ishirini (Tarawehe) na rakaa tatu za Witri”.

Na mjumuisho baina ya riwaya hizi unamkinika kwa khitilafu za hali. Na inawezekana kwamba khitilafu hiyo ni kwa sababu ya urefushaji wa kisomo na ufupishaji wake. Kwa hivyo basi, pale kinapo refushwa kisomo, idadi ya rakaa (nayo) hupungua na kinyume chake pia”. [FAT-HUL-BAARIY: 04/252, 253]

 

  

 | Tuandikie |