Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI-I

Faida

Fadhila za swaumu – I

           Wapendwa wetu katika imani-Allah aithibitishe imani yenu. Baada ya utafiti mfupi tulioufanya kwa msaada na taufiq ya Allah, tumegundua kwamba kuna baadhi ya waislamu hawafungi swaumu ya Ramadhani. Hawafungi kwa sababu wana udhuru wa kisheria unao wahalalishia kula, la hasha. Bali hawafungi kwa sababu:

F       Hawakulelewa katika misingi/malezi ya kidini tangu walipokuwa wadogo, hili likapelekea wao kutokuijua dini yao na hivyo basi kutokuyathamini maamrisho/makatazo yake.

F       Hawajui ubora/fadhila za ibada wanazo amrishwa kuzitekeleza.

Kwa kuzizingatia sababu mbili hizi kuu, tumeonelea ni vema tukaitumia fursa hii kwa msaada wa Allah, kubainisha baadhi tu ya fadhila za ibada tukufu ya swaumu. Tukitaraji kuwa, waja wa Allah wakizijua fadhila hizo, ujuzi wao huo utawasukuma kupania na kujipinda kuzivuna kheri zitokanazo na ibada hii tukufu ya swaumu ya Ramadhani. Kwa jina lake Taala tunasema: Katika jumla ya fadhila/ubora wa ibada ya swaumu ni kwamba:

1)      ALLAH TAALA AMEITEGEMEZEA NAFSI YAKE:

            Ibada ya swaumu ndio ibada pekee miongoni mwa ibada zote iliyopata utukufu wa kuambiwa na Allah Taala: “Swaumu ni yangu mimi”. Hivyo ndivyo ilivyothibiti katika hadithi – Qudsiy: “Kila amali ya mwanadamu ni yake yeye ila swaumu, hakika hiyo ni yangu mimi na mimi ndiye nitakayeilipa”. Muslim-Allah amrehemu.

Kauli hii tukufu ya Allah Taala, kama itakuwa inafahamisha na kuashiria jambo, basi jambo hilo halitakuwa jingine zaidi ya kuonyesha utukufu/ubora/daraja na cheo cha ibada hii adhimu ya swaumu. Ni kwa ajili hii, ndipo pale Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-aliposema: Ewe Mtume wa Allah, niamrishe kufanya amali, Mtume-Rehema na Amani zimshukie-akamwambia: “Jilazimishe kufunga, kwani hiyo (swaumu) haina hesabu (katika malipo yake)”. Muslim-Allah amrehemu.

Na hivyo – Allah ndiye Mjuzi mno – ni kwa sababu ya uficho wa amali uliomo ndani ya swaumu, kiasi cha kuwa ni siri baina ya Allah na mja wake tu. Swaumu ni amali ya batini isiyojulikana hakika yake ila na Allah Taala na ni amali pekee isiyokubali kuingiliwa na riyaa kama ilivyo kwa baki ya amali nyingine. Kwa mantiki hii, swaumu ndio amali ambayo ikhlasi hujidhihirisha humo sana kuliko katika amali nyingine. Kipande hiki cha hadithi ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-ni kielelezo kizuri cha ikhlasi ndani ya swaumu: “...huacha matamanio yake na chakula chake kwa ajili yangu...”. Kwa hivyo basi, mfungaji huwa hakusudii wala kulenga lo lote katika swaumu yake zaidi ya kupata radhi ya Mola wake Mtukufu. Yuko peke yake chumbani, njaa inamkwangua na kiu kinamuunguza, chakula anacho na maji anayo na hakuna jicho limuonalo. Kwa nini basi asile wala kunywa?! Ni kwa sababu ya ikhlasi iliyomjaa akilini, moyoni na mwilini tu basi. Ni ikhlasi hiyo ndio inayompa hisia na imani kuwa yeye kafunga kwa ajili ya Allah Mola Muumba na sio kwa ajili ya watu. Sasa ni kweli humo chumbani watu hawamuoni, hata akila au kunywa hawatajua, lakini Allah Taala aliyemuamrisha kufunga anamuona na ni Yeye ndiye atakayemlipa juu ya ibada yake hiyo na wala si watu.

2)      MFUNGAJI HULIPWA UJIRA WAKE PASIPO NA HESABU:

            Allah Taala ametaja ujira wa amali nyingine zisizo swaumu, kwamba mja akitenda amali kadha moja atalipwa kumi mfano wake mpaka mia saba maradufu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zismhukie-amesema: “Kila mwanadamu hurudufishiwa jema kwa kumi mfano wake (jema hilo) mpaka mia saba maradufu”. Allah Taala nae akasema: “...ila swaumu, hakika hiyo (swaumu) ni yangu nami ndiye niilipaye...” Muslim-Allah amrehemu.

Allah Taala atakapoitawalia jazaa/ujira wa ibada hii ya swaumu, basi yeye ni Karimu mno ambaye vipawa na upaji wake hauna ukomo/mpaka. Na hayo ndio malipo/ujira wa wenye kusubiri, kwani hakika swaumu ni katika subira, Allah Taala amesema: “...NA BILA SHAKA WAFANYAO SUBIRA (wakajizuilia na maasi na wakaendelea kufanya ya twaa) WATAPEWA UJIRA WAO PASIPO HESABU”. [39:10] Imamu Auzaaiy-Allah amrehemu amesema: “Hawatapimiwa (ujira wao) kwa mizani wala kilo, hakika si vinginevyo watachotewa (tu) mchoto”.

3)      SWAUMU NI KINGA DHIDI YA MATAMANIO MAOVU:

            Ni maumbile ya nafsi ya mwanadamu kupenda mno kutenda maovu kama alivyosema Allah Taala: “...KWA HAKIKA (kila) NAFSI NI YENYE KUAMRISHA SANA MAOVU, ISIPOKUWA ILE AMBAYO MOLA WANGU AMEIREHEMU...” [12:53] Hayo ndio maumbile na matashi ya kila nafsi, kwa kulitambua hilo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatuelekeza kuyavunja na kuyazima matamanio kwa kutumia silaha ya swaumu, akasema: “Enyi kusanyiko la vijana! Ye yote miongoni mwenu atakayeweza kuangalia nyumba, basi na aoe, kwani huko (kuoa) kunalihifadhi mno jicho na kunaipa ngome tupu. Na asiyeweza (gharama za nyumba), basi na ajilazimishe na swaumu, kwani hiyo (swaumu) ni kinga kwake (dhidi ya maasi)”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu. Na ni kweli kabisa aliyoyasema Bwana Mtume, kwani imethibiti kupitia majaribio kwamba swaumu inapunguza matamanio kwa kiwango kikubwa sana, kama sio kuyakata kabisa.

4)      SWAUMU NI KINGA DHIDI YA KAULI ZA POROJO NA MATENDO YA KIPUUZI:

           Muislamu mkamilifu wa imani ni yule anayeithamini kila pumzi ya uhai wake, kwa kutambua kuwa hiyo ndio rasilimali yake. Haipotezi rasilimali yake hii katika baraza za porojo wala katika kutenda matendo ya kipuuzi yasiyomnufaisha kwa cho chote katika dunia wala akhera yake. Lakini Allah Taala kwa kutambua kuwa hayo ndio yapendwayo na mwanadamu, akamuwekea ibada ya swaumu ili impe kinga dhidi ya mambo hayo yasiyo mnufaisha wala kumfaidisha. Mtume wa Allah-Rehama na Amani zimshukie-amesema: “...na swaumu ni kinga, atakapofunga mmoja wenu asiseme maneno machafu siku hiyo na wala asipayuke. Iwapo mtu atamtukana au kumpiga, basi na aseme hakika mimi nimefunga”. Muslim-Allah amrehemu.

Mfungaji kukatazwa kusema maneno machafu na kupayukapayuka hovyo, kuna msaada mkubwa kwake katika kuidhibiti nafsi yake; ulimi, viungo na moyo wake dhidi ya kutenda maasi.

5)      SWAUMU NI KINGA NA SITARA DHIDI YA ADHABU KALI YA MOTO:

          Sote tunaamini kwamba Allah Taala ameiandaa pepo na moto (jahanamu) huko akhera. Pepo yake tukufu amewaandalia waja wake wema watakaoishi hapa duniani kwa kuufuata muongozo wake. Na moto amaeuweka tayari kwa wale wote watakaoukhalifu muongozo wake huo, tusome: “TUKASEMA: SHUKENI HUMO NYOTE; NA KAMA UKIKUFIKIENI UWONGOZI UTOKAO KWANGU, BASI WATAKAOUFUATA UWONGOZI WANGU HUO HAITAKUWA KHOFU JUU YAO WALA HAWATAHUZUNIKA. LAKINI WENYE KUKUFURU NA KUYAKADHIBISHA MANENO YETU, HAO NDIO WATAKAOKUWA WATU WA MOTONI, HUMO WATAKAA MILELE”. [2:38-39]

Naam, ni kweli kabisa kuwa adhabu kali ya moto ipo na ipo kwa ajili tu ya watakao zikhalifu amri za Mola wao. Sasa basi mojawapo ya mambo yatakayokusaidia kuiepa adhabu kali hii ya moto kwa fadhila zake Allah ni ibada hii ya swaumu. Kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Swaumu ni kinga na ni ngome madhubuti dhidi ya (adhabu ya) moto”. Ahmad-Allah amrehemu. Na katika hadithi nyingine Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Atakayefunga siku moja katika njia ya Allah, Allah atauepusha uso wake na moto kwa matapo sabini”. Muslim-Allah amrehemu. Kila swaumu inahesabika kuwa iko katika njia ya Allah, pale itakapokuwa ni kwa ajili ya Allah tu kama walivyosema hivyo baadhi ya wanachuoni.

Hali kadhalika, Allah huwaneemesha baadhi ya wafungaji kwa kuwaacha huru na adhabu ya moto kama alivyosema Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Hakika Allah Taala anao waachwa huru na moto wakati wa kila kufuturu na hilo (hupatikana) katika kila usiku”. Ahmad-Allah amrehemu.

6)      SWAUMU NI NJIA YA KUENDEA PEPONI:

          Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-kwamba yeye alisema: Ewe Mtume wa Allah, niamrishe jambo litakalonifaa. (Mtume) akasema: “Shikamana na swaumu, kwani hiyo (Swaumu) haina mfano wake”. Muslim-Allah amrehemu. Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amebainisha kupitia kauli yake hii, kwamba hapana kitu kinachomkurubisha zaidi mja kwa Mola Muumba wake na kumuepusha na moto kama swaumu. Na katika kuonyesha ukarimu wake kwa wafungaji, Allah Taala akawawekea wafungaji mlango maalumu peponi, ambao humo hataingia ila mfungaji tu. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Hakika peponi kuna mlango unaoitwa RAYYAAN, wataingia humo wafungaji siku ya Kiyama. Hataingia humo ye yote asiye wao, patasemwa: Wako wapi wafungaji? Watainuka, hataingia humo ye yote asiye wao, watakapoingia (mlango) utafungwa na hataingia humo ye yote”.

Walipostahamili machungu na joto la kiu kwa ajili ya Allah Taala, nae akawaingiza peponi kupitia mlango huo RAYYAAN, kwani jazaa hutegemeana na hulingana na amali iliyo tendwa. Na joto linapomzidia mfungaji ndivyo ujira navyo unavyozidi, Allah atamlipa na kumnywesha katika siku hiyo ya kiu kali. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abbas-Allah awawiye radhi-kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimtuma Abu Mousa na sariya (kikosi cha askari) baharini. Basi wakati wako hivyo wakiwa wameinua tanga katika usiku wa giza, tahamaki wakasikia sauti ikisema: Enyi watu wa jahazi, simameni nikuambieni hukumu ya Allah aliyoihukumia nafsi yake. Abu Mousa akasema: “Haya tukhabarishe ikiwa wewe ni mkhabarishaji. Ikasema (sauti): Hakika Allah Taala ameihukumia nafsi yake, kwamba ye yote atakayeitia kiu nafsi yake katika siku ya joto kali, Allah atamnywesha siku ya kiu”. [SAHIHUT-TARGHIYBU WAT-TARHIYBU].

7)      HARUFU YA KINYWA CHA MFUNGAJI NI NZURI ZAIDI MBELE YA ALLAH KULIKO HARUFU YA MISKI:

          Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Naapa kwa yule ambaye nafsi ya Muhammad i mkononi mwake, kwa yakini harufu ya kinywa cha mfungaji yapendeza mno mbele ya Allah siku ya Kiyama kuliko harufu ya miski”. Hapo zitakapo dhihiri thawabu za amali kwani huo ndio wakati wa kudhihiri athari ya ibada. Hadithi hii ya Bwana Mtume, inafahamisha kwamba athari itokanayo na ibada ni miongoni mwa vitu anavyovipenda Allah Taala. Na hili linatuwekea wazi mapenzi makubwa ya Allah Taala katika kuipenda amali njema na hali ilivyo mtumwa hupupia na kupania kutenda kila amali impendazayo Bwana wake ili apate mkuruba wake.

8)      SWAUMU HURITHISHA MAFANIKIO DUNIANI NA AKHERA:

           Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-anasema: “Mfungaji ana furaha mbili; furaha wakati wa kufuturu kwake na furaha wakati wa kukutana na Mola wake”. Bukhaariy & muslim-Allah awarehemu.

Furaha ya muumini mfungaji wakati wa kufuturu kwake hupatikana kwa ajili ya kufurahikia kuwafikishwa na Allah kuikamilisha swaumu ya siku hiyo. Na hufurahi pia kwa sababu Allah Taala amemuhalalishia kula na kunywa na hivyo ni miongoni mwa vitu vinavyopendwa mno na nafsi. Na huu ni mfano wa ladha na mafanikio ya kweli anayo yapata muumini kwa sababu ya kumtii kwake Mola wake.

9)      SWAUMU NI MUOMBEZI WA MFUNGAJI SIKU YA KIYAMA:

            Imepokewa kutoka kwa Abdullah Ibn Amrou-Allah amuwiye radhi-kwamba Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Swaumu na Qur-ani vitamuombea mja siku ya Kiyama. Swaumu itasema: Ewe Mola wangu! Mimi nilimnyima chakula na matamanio yake wakati wa mchana, basi nikubalie uombezi wangu kwake. Na Qur-ani itasema: Ewe Mola wangu! Nilimnyima kulala usiku, basi nikubalie uombezi wangu kwake. (Mtume) akasema: Basi zitakubaliwa uombezi wao”. Ahmad-Allah amrehemu.

10)         SWAUMU NI KAFARA NA KIFUTIO CHA DHAMBI:

               Ibada tukufu ya swaumu inakuwa kafara na kifutio cha dhambi, kwa sababu inajumuisha na kukusanya ndani yake mema mengi, na Allah Taala amesema: “...HAKIKA MEMA HUONDOA MAOVU. HUU NI UKUMBUSHO KWA WANAOKUMBUKA”. [11:114] Na zimepokewa hadithi nyingi zinazobainisha kuwa swaumu ni kifutio cha dhambi, miongoni mwa hizo ni kauli yake Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Fitna ya mtu kwa mkewe, mali yake na jirani yake, hufutwa na swala, swaumu na sadaka”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Yaani kila makosa anayoyafanya mtu kwa upande wa haki ya mkewe, wanawe na jirani yake kutokana na maneno yake mabaya au haki za kimali. Dhambi zitokanazo na makosa hayo hufutwa na thawabu za ibada ya swala,  swaumu na sadaka. Na swaumu ya Ramadhani ndio inayokhusika zaidi na ufutaji wa dhambi, kama lilivyothibiti hili katika kauli ya Mtume-Rehema na Amani zimshukie: “Atakayefunga (swaumu ya) Ramadhani kwa imani na kwa kutaraji malipo kutoka kwa Allah, atasamehewa dhambi zake zilizotangulia”. Bukhaariy & Muslim-Allah awarehemu.

Na katika hadithi nyingine, Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Swala tano (swala ya) Ijumaa mpaka Ijumaa na (swaumu ya) Ramadhani mpaka Ramadhani, ni kafara ya madhmabi yaliyo baina yao pale yatakapoepukwa madhambi makubwa”. Muslim-Allah amrehemu.

Kwa kauli hii ya Bwana Mtume, inatuwazikia kumbe swaumu hufuta madhambi madogo madogo na wala sio yale makubwa. Madhambi makubwa hayafutwi ila na toba, Allah Taala anasema: “KAMA MKIJIEPUSHA NA MAOVU MAKUBWA MNAYOKATAZWA. TUTAKUFUTIENI MAKOSA YENU MADOGO NA TUTAKUINGIZENI MAHALI PATUKUFU (kabisa, napo ni peponi)”. [4:31]

Hadithi mbili tulizozinukuu na aya hii tukufu zimefahamisha kwamba ili kuyapata maghfira (msamaha) ya Allah, ni lazima zipatikane sharti tatu hizi zifuatazo:

                     i.            Kufunga swaumu ya Ramdhani kwa kumuamini Allah na Mtume wake na kusadikisha ufaradhi wa ibada ya swaumu na ujira aliowaandalia Allah waja wake wafungaji.

                   ii.            Afunge Ramadhnai kwa kutarajia ujira kutoka kwa Allah Taala ilhali akiwa mwenye ikhlasi kwake.

                  iii.            Kujiepusha na madhambi makubwa, na haya ni kila dhambi ambayo inapotendwa huandamiwa na adhabu “haddi” hapa duniani au makamio akhera au na ghadhabu au laana ya Allah na mfano wake. Madhambi ya namna hiyo ni kama vile shirki, kula riba, kula mali ya yatima, zinaa, uchawi, kuua, kuwaasi wazazi, kukata udugu, kutoa ushahidi wa uongo, ghushi (utapeli), kusengenya, kuficha haki na kadhalika.

Naam, ndugu mpendwa katika Allah, tayari umekwishaona fadhila/ubora wa swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Hebu sasa na tujiulize:

Je, ni swaumu ipi ndio inaweza kumpatia muislamu fadhila hizi adhimu?

          Fadhila zote ambazo tumezitaja kuwa zinapatikana ndani ya ibada ya swaumu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, hatazipata ila yule atakayefunga kwa sharti zifuatazo:

                   i.            Awe na ikhlasi katika swaumu yake; yaani afunge tu kwa ajili ya Allah Taala, hasikusudie ila kupata radhi za Allah. Asifunge kwa ajili ya kuonekana/kusifiwa na watu, kwa ujumla asifunge kwa ajili ya kupata malengo yake ya kudunia.

                 ii.            Swaumu yake yote ifuate muongozo wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-; yaani afunge kama alivyofundisha Bwana Mtume.

                iii.            Viungo vyake navyo vyote vifunge; yaani avizuie na yale yote yaliyoharamishwa. Ulimi wake ufunge, usiseme uongo, kusengenya, kutoa maneno machafu na.... na.... Jicho lake nalo lifunge, lisiangalie vilivyo haramishwa. Sikio nalo pia lifunge, lisisikilize muziki na kila lililo haramishwa. Mkono nao pia ufunge, usile haramu, usipige pasina haki na mguu nao ufunge, uuzuie kwenda katika mambo ya haramu. Na haya ndio malengo makuu ya ibada ya swaumu, kwa ajili hii basi swaumu imekuwa ndio chuo cha kulea nafsi katika mambo matukufu/mema na kumuepusha na mambo maovu/mabaya.

Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-amesema: “Ambaye hakuacha maneno ya uongo na kuyafanyia kazi na (hakuacha) upuuzi, basi Allah hana haja katika kuacha kwake chakula na kinywaji chake”. Muslim-Allah amrehemu.

Na katika hadithi nyingine, amesema: “Huenda mfungaji, fungu lake katika swaumu yake (likawa ni) njaa (tu) na kiu. Na huenda msimamaji (usiku kufanya ibada), fungu lake kutokana na kisimamo chake hicho (likawa) ni kukesha (tu)”. Ahmad-Allah amrehemu.

 

  

 | Tuandikie |