Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

Nasaha za Dini  

"Dini ni nasaha, wakauliza kwa nani ? Akasema Mtume : Kwa Allah, Mtume wake, kwa viongozi wa waislamu na watu wa kawaida" Hadith Tukufu

MINBARI YA RAMADHANI 03

Faida

 

     01.       Swala ya Tarawehe; Hukumu na Fadhila/Ubora wake:

         Haya na tuanze sasa tuliyo yaazimia; yaani kubainisha Muongozo wa Mtume katika swala ya Tarawehe. Basi tunasema hali ya kuwa tunataka auni (msaada) na taufiq kutoka kwa Allah:

         Swala ya Tarawehe, ni swala inayo tekelezwa (swaliwa) katika usiku wa mwezi mtukufu wa Ramadhani baada ya (kuswaliwa) swala ya Ishaa na kabla ya swala ya Witri.

(Swala hii), ni SUNNA kwa upande wa wanaume na wanawake, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliiswali na akaidumisha na akawahimiza watu kuitekeleza. Na wakaidumisha maswahaba na Taabiina baada yake.

Na swala hii ni nembo miongoni mwa nembo za mwezi mbarikiwa wa Ramadhani, swala hii ina utukufu wake ndani ya nafsi za Waislamu. Kama ambavyo ina heshima na ubora wake kwa Mola Mlezi wa viumbe wote.

Imekuja katika hadithi sahihi ambayo ameitaja Imamu Bukhaariy, (imepokewa) kutoka kwa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie: “Atakaye simama (usiku kuswali) ndani ya mwezi wa Ramadhani, kwa imani na kwa kutaraji malipo (kutoka kwa Allah). Atasamehewa yaliyo tangulia katika madhambi yake”.

Na maana ya hadithi hii tukufu: Ni kwamba yule atakaye uhuisha usiku wa Ramadhani kwa swala, dhikri na kusoma Qur-ani, hali ya kumuamini Allah na kutarajia kupata ujira na thawabu zake kutoka kwake. Allah atamsamehe dhambi zake zilizo pita; zile dhambi ndogo miongoni mwake. Ama yale madhambi makubwa, hapana budi yaletewe toba isiyo rejewa rejewa, kama walivyo lifumbuliza hilo wengi miongoni mwa Mafaqihi. [Angalia, AL-FIQ-HUL-WAADHWIHU ALAL-MADHAAHIBIL-ARBAA cha Dk. Muhamad Bakri Ismail 3/25]

 

     02.       Wa mwanzo kuswali Tarawehe ni Mtume wa Allah:

         Amesema Ibn Qudaamah-Allah amrehemu-katika kitabu chake “AL-MUGHNIY”, maneno ambayo nukuu yake ni: “Nayo (hiyo Tarawehe) ni SUNNA kokotezwa na wa mwanzo kuianzisha Sunna hii ni Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie.

(a)     Amesema Sayyidna Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi: (Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiraghibisha katika kisimamo cha Ramadhani, bila ya kuwaamrisha kutinda katika hicho (kisimamo kwa rakaa maalumu), akisema: “Atakaye simama (usiku kuswali) ndani ya mwezi wa Ramadhani, kwa imani na kwa kutaraji malipo (kutoka kwa Allah). Atasamehewa yaliyo tangulia katika madhambi yake”). Muslim-Allah amrehemu.

(b)    Na amesema Bi. Aysha-Allah amuwiye radhi: (Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-aliswali msikitini usiku mmoja, watu wakaswali kwa swala yake (wakamfuata wakaswali jamaa pamoja nae). Kisha akaswali usiku ulio fuatia, watu wakaongezeka zaidi. Kisha wakakusanyika katika usiku wa tatu au wanne, basi Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakuwatokea. Kulipo pambazuka akasema: “Hakika niliona ambacho mlikitenda (kukusanyika kwenu), basi hakukunizuia kukutokeeni ila ni kwamba mimi nilichelea isije ikafaradhishwa juu yenu”. – Na hilo lilikuwa ndani ya Ramadhani. [SAHIH MUSLIM 1/524]

(c)     Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayrah-Allah amuwiye radhi-amesema: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka katika Ramadhani tahamaki watu wakiswali katika upande mmoja wa msikiti, akauliza: Hawa ni kina nani? Akajibiwa: Hawa ni watu wasio hifadhi Qur-ani, Ubayyu Bin Ka’ab anaswalisha nao wanaswali kwa swala yake (wanamfuata). Hapo ndipo Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akasema: Wamesibu (wamepatia) na mazuri/bora yaliyoje waliyo yatenda”. Abu Daawoud-Allah amrehemu.

Na swala ya Tarawehe imenasibishwa na Sayyidna Umar Bin     Al-Khatwaab-Allah amuwiye radhi-kwa sababu yeye ndiye aliye wakusanya watu kuswali nyuma ya “Sayyidna Ubayyu Bin Ka’ab”. Akawa yeye ndiye (Imamu) anawaswalisha.

Imamu Bukhaariy-Allah amrehemu-amepokea kutoka kwa Abdurahman Bin Abdil-Qaariy-amesema: “Nilitoka kwa Umar Bin Al-Khatwaab katika usiku mmoja wa Ramadhani, tahamaki hao ni watu vipote vipote – yaani wanaswali makundi makundi – tapanyi. Mtu anaswali peke yake na mtu mwingine anakiswalisha kikundi cha watu (wachache). Umar akasema: Hakika mimi naona lau ninge wakusanya watu hawa nyuma ya msomaji mmoja, ingeli kuwa bora zaidi. Kisha akaazimia na akawakusanya nyuma ya (Ubayyu Bin Ka’ab). Anasema (msimulizi): Kisha nikatoka nae usiku mwingine na ilhali watu wakiswali kwa swala ya msomaji wao. Hapo ndipo Umar alipo sema: Bora ya bidaa ni hii. Na (swala) ambayo watu wanailaza ni bora zaidi kuliko ile wanayo simama (kuswali mapema) – anakusudia (ile inayo swaliwa) mwisho wa usiku. Na watu walikuwa wakisimama mwanzo wake (usiku)”. [AL-MUGHNIY Ya Ibn Qudaamah]

Kutokana na hadithi hizi tukufu, inatubainikia kwa uwazi, kwamba wa kwanza kuiswali Swala ya Tarawehe katika kisimamo cha Ramadhani, ni Bwana wetu Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Aliwaswalisha (maswahaba) siku tatu au nne, kisha hakuwatokea tena baada ya hapo, kwa kuwaonea huruma. Kwa sababu yeye (Mtume)-Rehema na Amani zimshukie-alichelea isije ikafaradhishwa juu yao. Na hii (hadithi) inatiwa nguvu na ile iliyo pokewa na maimamu Bukhaariy na Muslim kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alitoka ndani ya usiku mwingi – na hiyo ilikuwa ni ndani ya Ramadhani. Akaswali msikitini, basi watu wakaswali kwa swala yake (wakamfuata). Watu wakapambazukiwa wakilizungumza hilo, kwa ajili hiyo wakakusanyika wengi kuliko wale (wa jana). Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akatoka katika usiku wa pili, akawaswalisha. Watu wakapambazukiwa wakilitaja hilo, wakakithiri wadau wa msikiti katika usiku wa tatu. Mtume akatoka, watu wakaswali kwa swala yake. Ulipo fika usiku wa nne, msikiti ukafurika na kutapika watu, Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakuwatokea. Watu wakaanza kusema: Swala! Swala! Bado Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-hakutoka mpaka akatoka kwa ajili ya swala ya Alfajiri. Ilipo kwisha swaliwa Alfajiri, aliwaelekea watu, akatoa shahada, akasema: “Ama baad, hakika ya hali halikufichika kwangu jambo lenu la usiku wa kuamkia leo. Lakini mimi nimechelea kufaradhishwa juu yenu swala ya usiku, kisha ikakushindeni”. [Bukhaariy 3/220]-Allah amrehemu-na angalia [JAAMIUL-USUUL 6/117]

Na katika riwaya nyingine: “Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akafa na hali ikiwa hivyo”.

“Neno TARAWEH ni wingi wa neno TAR-WIYHAH, nayo (Tar-wiyhah) maana yake ni mara moja ya raha/mapumziko. (Neno hili ni) mfano wa neno TASLIYMAH kwa neno SALAAM. Na TAR-WIYHAH katika mwezi wa Ramadhani, imeitwa hivyo kwa sababu ya kupumzika watu baada ya kila rakaa nne. Kisha akasema: Na neno RAAHAH (raha/mapumziko) ni kinyume cha neno TA’AB (shida/taabu). Na (imekuja) katika hadithi kwamba Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alimwambia Bilali: “Tupe raha/tustareheshe kwayo ewe Bilali!” – Yaani adhini kwa ajili ya swala, tupate raha (kustarehe) kwa kuitekeleza. Akawa (Mtume) anapata raha kwa kuswali kutokana na kunong’ona na Allah kulikomo humo, ni kwa ajili hii ndipo alipata kusema: “Na nimejaaliwa burudani (tuzo) ya macho yangu ndani ya swala”. [LISAANUL-ARAB, Juz. 1]

Kwa maelezo haya basi, swala ya Tarawehe ndio swala ya “Kisimamo cha Ramadhani”, kama ilivyo thibiti katika hadithi sahihi ambazo tumezitaja.

  

 | Tuandikie |