|
SOMO LA TATU.
I.
Khabari za Al-Aswad:
Waislamu walipo ifungua nchi ya Yemen na kuwa chini
ya himaya ya mamlaka ya Kiislamu, katika zama za Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie. Mtume akamtawadha Baadhaan Al-Faarisiy kuwa gavana wa
Yemen, huyu ni Mfursi wa Iran ambaye alipelekwa Yemen na Kisraa (mfalme)
Abrawiyz kuwa gavana huko kwa niaba yake. Akaendelea kumuwakilisha Kisraa
huko mpaka Mtume wa Allah alipo twaa madaraka ya huko, nae ndiye aliye funga
ukurasa wa magavana wa Kifursi walio itawala Yemen. Baada ya utawala wa
Yemen kuangukia mikononi mwa waislamu, Baadhaan akasilimu na ndipo Mtume
akambakisha katika wadhifa wake wa ugavana. Na makao yake makuu yalikuwa
katika mji wa Sanaa. Aliendelea na wadhifa wake huo mpaka alipo fariki
dunia. Alipo kufa Mtume wa Allah akayagawanya madaraka yake. Akampa ugavana
wa mji wa Yemen mwanawe; Shahri Ibn Baadhaan. Abu Mousa Al-Ash’ariy
akatawazwa kuwa gavana wa mji wa Ma’arab. Ugavana wa mji wa Hamdaan akapewa
Aamir Ibn Shahri Al-Hamdaaniy, mji huu ulikuwa mashariki mwa Yemen. Twaahir
Ibn Haalah akatawalishwa kwa makabila ya Aki na Ash-ariyin, ukoo wa Aki
ulikuwa ukiishi baina ya miji ya Zabeed na Rumui. Na huyu mzee Aki ni mtoto
wa Adnaan. Na Waash’ari walikuwa wakiishi kaskazini mwa mji wa Zabeed na
wananasibishwa na Ash’ari Ibn Adad Ibn Zaid Ibn Yashjab Ibn Ariyb Ibn Zaid
Ibn Kahlaan. Khalid Ibn Said Ibn Al-Aaswi yeye akapewa ugavana wa eneo
lililo baina ya miji ya Najiraan, Rumui na Zabeed. Amrou Ibn Hazm akawa
gavana wa Najiraan, mji wa Hadharamout akatawalishwa Ziyaad Ibn Labeed
Al-Bayaadhiy. Ukaashah Ibn Thaur akasimikwa ugavana wa makabila ya Sakaasik
na Sukuun, haya ni makabila ya Kandah yaliyo kuwa yakiishi kaskazini mwa mji
wa Hadharamout. Al-Muhaajir Ibn Umayah ndugu wa mama wa waumini; Ummu
Salamah, akateuliwa kuwa gavana wa ukoo wa Muawiyah. Lakini hakwenda kukalia
kiti chake hicho mpaka Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo
fariki, kwa sababu ya maradhi aliyo kuwa nayo. Ziyaad Ibn Labeed akakaimu
ugavana kwa niaba yake. Ya’alaa Ibn Umayah yeye akapewa ugavana wa Al-Jundi.
Muaadh Ibn Jabal akapewa wadhifa wa ualimu, akawa akiuzungukia mji baada ya
mwingine.
Muda mchache kabla ya kifo cha Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-mtu mmoja wa kabila la Unsi aitwaye Ab-halah. Mwenye lakabu
ya “Dhul-Khimaar”, akijulikana zaidi kwa jina la Al-Aswad, akaleta machafuko
Yemen kwa kudai utume. Madai yake hayo yakaitikiwa kwa mikono miwili na watu
wa kabila la Mudh-haj. Alipo pata uungwa mkono huu, akaenda kuuvamia mji wa
Najiraan akamng’oa madarakani gavana wake; Amrou Ibn Hazmi. Pia akamuondosha
madarakani Khalid Ibn Said Ibn Al-Aaswi, magavana wawili hawa wakatoroka
wakaenda Madinah. Al-Aswad hakuushia hapo, akatoka na watu mia saba wa
kabila lake, wakaelekea Sanaa. Huko akamuua gavana Shahri Ibn Baadhaan na
kukalia kiti chake na akamuoa kwa nguvu mjane wa marehemu. Akatawalia eneo
lote lililo baina ya Sanaa na Hadharamout kwa upande wa Kaskazini mpaka
Bahrein kwa upande wa Mashariki. Nguvu yake ikawa kubwa, Muaadh Ibn Jabal
kuona hivyo akatoka hali ya kukimbia, akampitia Abu Mousa katika mji wa
Ma’arab. Akatoka pamoja nae, wakaenda Hadharamout, Muaadh akashukia katika
kabila la Sakaasik na Abu Mousa akawa mgeni wa kabila la Sukuun. Gavana
Twahir Ibn Abu Haalah, yeye akabakia katika mji wa kabila la Aki.
Khabari za tukio hilo zilipo mfikia Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-akawapelekea ujumbe vijana wa Kiislamu wa Yemen, na magavana
Abu Mousa, Muaadh na Twahir. Ya kwamba wachukue jukumu la kumuua Nabii wa
uwongo; Al-Aswad. Vijana Feiruz na Daadhawiyhi wakalibeba jukumu hilo,
wakapanga mipango ya kumuua wakisaidiwa na mke wake ambaye alimuoa kwa nguvu
baada ya kumuua mumewe; gavana Shahri Ibn Baadhaan. Hata mipango ilipo iva,
wakafanikiwa kumuua usiku, Feiruz ndiye aliye muua usiku. Kulipo pambazuka
asubuhi wakapiga mbiu mgambo ya Kiislamu, nayo ni adhana, waislamu wakaja
kama mawimbi ya bahari. Kuona hivyo, wafuasi wa Al-Aswad wakawakwapua baadhi
ya watoto wa waislamu kama ngao, wakatoka mjini wakiwaacha nyuma wengi
miongoni mwa watoto wao. Kisha pande mbili hizi; kundi la Mtume wa haki na
lile la Mtume wa uwongo, zikatumiana ujumbe ya kwamba kila upande urejeshe
watoto wa upande mwingine. Baada ya kutekelezwa matakwa haya kwa kila
upande, wafuasi wa Al-Aswad wakawa wakitangatanga baina ya Sanaa na Aden.
Baada ya hali kurejea shwari, magavana wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakarejea kwenye nyadhifa zao. Na
wakawafikiana ya kwamba mwalimu Muaadh ashike makamu ya kuwaswalisha watu
Sanaa kufuatia kuuawa kwa gavana wake; Shahri mpaka yaje maelekezo mengine
kutoka kwa Mtume wa Allah. Wakapeleka taarifa za kadhia yote Madinah; makao
makuu ya Dola ya Kiislamu. Mjumbe akawasili Madinah ilhali tayari Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-akiwa ameshaaga Dunia na khalifa Abu Bakri
kushika makamu yake. Ikawa hii ndio khabari njema ya kwanza ya ushindi wa
Uislamu kumfikia Amirul-Muuminina; Abu Bakri.
Khabari za kifo cha Mtume zilipo tangaa, Qays Ibn Abdi
Yaghuuth akaritadi na akawaandikia waraka washindwa katika jeshi la mtume wa
uwongo; Al-Aswad. Wakajikusanya kwake, akala njama ya kuwaua wakubwa wa
vijana, nao Feiruz, Daadhawiyhi na Khashanshi. Akawaandalia karamu,
akawaalika wote ili apate kuwaua kwa hila, akafanikiwa kumuua Daadhawiyhi na
wenzake wawili wakaponyoka. Akatoka kuwafuatia, nao wakakimbia na kwenda
kuomba hifadhi kwa kabila la Khaulaan. Hapo ndipo zilipo komelea mbio za
Qays, akarejea Sanaa akajiimarisha hapo. Akaziendea familia za vijana wale,
akawaghuri na kuwatoa Yemen barani na baharini na kuwatishia amani. Feiruz
alipo pata khabari hizo akakusudia kumpiga vita, akaomba msaada kwa makabila
ya Aqeel Ibn Rabeeah na Aki. Wakamuendea na kufanikiwa kuzikomboa familia
alizo kuwa ameziteka Qays na kuwaua watu wake alio kuwa nao.
Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, wakaelekea kwa Feiruz,
akawaongoza kupambana na Qays na watu wake mpaka wakawashinda. Na ni katika
kipindi hicho aliwajia Muhaajir Ibn Umayah ambaye Sayyidna Abu Bakri
alimsimikia bendera na kumpeleka kupambana na majeshi ya Al-Aswad na
kuwasaidia wale vijana. Na akafuatiwa na Ikrimah Ibn Abu Jahli baada ya
kumaliza kazi aliyo tumwa kuifanya Oman na Mahrah. Wote wawili hawa
wakawasaidia vijana kupambana na majeshi ya Qays Ibn Abdi Yaghuuth.
Wakapigana nao mpaka wakawashinda na kuwatwaa mateka Qays na Amrou Ibn Ma’ad
Yakrib Az-zabeediy ambaye alikuwa ameritadi na kumfuata Al-Aswad.
Wakawapeleka Madinah kwa khalifa Abu Bakri-Allah amuwiye radhi.
Walipo fikishwa kwa khalifa Abu Bakri, akasema: Ewe Qays!
Umewaua waja wa Allah na ukawafanya waritadi kuwa ndio watu wako wa karibu
na wasiri wako kinyume na waumini. Qays akakanusha kushiriki kwa lolote
katika kadhia ya Daadhawiyhi na haukuwepo ushahidi wa wazi juu ya kumuua
kwake, kwa sababu mauaji yake yalikuwa ni ya kificho. Kwa unakushi wake huo
na kwa kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja utakao mtia hatiani, akawa
amejikosha na damu ya Daadhawiyhi iliyo mwagika. Na akamwambia Amrou Ibn
Ma’adi Yakrib; Hivyo wewe huoni haya kwamba wewe kila leo ama unashindwa au
unatekwa! Lau ungeli inusuru dini hii, bila ya shaka Allah angeli kunyanyua
daraja ya juu. Akasema: hapana ubaya, ninakubali makosa na sitarudia tena.
Baada ya kukiri huku, Amirul-Muuminina; Abu Bakri akawaacha huru, wakarejea
kwa jamaa zao hali ya kuwa ni waumini.
Baada ya hapo Al-Muhaajir Ibn Abu Umayah akayafuatilia
mabaki ya jeshi la Al-Aswad kila mahala na kuyafyekelea mbali kwa kila njia.
Ili yasiweze kusimama tena na kuleta usumbufu kwa waislamu. Na kipindi cha
nabii huyu wa uwongo; Al-Aswad tangu alipo dai utume mpaka anauawa, ilikuwa
ni miezi minne takriban. [Rejea AL-KAAMIL FIT-TAAREEKH 2/231 na AL-BIDAAYAH
WAN-NIHAAYAH 4/702].
|