Makala
Uislamu-Utangulizi
Fiqhi na Sheria 
Akhlaaq-Tabia
Sira ya Mtume
Nasaha za dini
Maswali na Majibu
Uliza Suala la dini
Jiunge na Mtandao !!!

 

SIRA YA MTUME (SAW)  

"BILA SHAKA MNAO MFANO MWEMA KWA MTUME WA MWENYEZI MUNGU…"Al-qur-an (33:21)

KHABARI ZA KANDAH

 Faida

 

    II.       Khabarari za Kandah:

         Watu wa Kandah walikuwa wameritadi katika zama za Nabii wa uwongo; Al-Aswad. Waliliritadi kwa sababu ya yaliyotokea baina yao na gavana Ziyaad Ibn Labeed katika kadhia ya faradhi ya Zakah. Kadhia hii ilitokana na makadirio ya zakah yaliyo kosewa na ikachochewa na watu wa kabila la Amrou Ibn Muawiyah hapo Kandah. Kwa sababu ya uritadi wao huu, ndipo gavana Ziyaad akakata shauri la kuwapiga vita, akawapiga na kuwashinda.

Baniy Muawiya wote wa Kandah wakawafikiana na kukongamana kuacha kutoa fungu la Zakah, ila Shurahbeelah Ibn As-samtw na mwanawe. Kwani wawili hawa waliwaambia Baniy Muawiya: “Hakika ni jambo baya kwa watu waungwana kubadili walicho kikubali. Hakika watu watukufu hujilazimisha na jambo la shubuha basi hupata utukufu kwa kuhamia jambo lililo wazi zaidi kuliko hilo (la shubuha). (Hufanya hivyo) kwa kuchelea aibu. Basi je, ni vipi (inakuwa) kuliacha jambo zuri na jema na kuiendea batili iliyo mbaya! Ewe Mola wa haki! Hakika sisi hatuiungi mkono kaumu katika hili”. Baada ya kwisha kuwaambia jamaa zao maneno hayo yenye busara na nasaha njema, wakaondoka kwenda kwa Ziyaad. Wakamwambia gavana: “Washambulie usiku watu hawa, ukitofanya hivyo tunachelea watu wasije wakachangukana nasi”.

Gavana Ziyaad kwa kuyazungatia maslahi ya uma, akaukubali ushauri wa Shurahbeelah na mwanawe. Akaandaa jeshi lake na kwenda kupambana nao katika ngome zao, akawakamata wafalme (viongozi) wao na akawaua. Na wakakimbia wale walio weza kukimbia, Waislamu wakarejea salama wakiwa wamepata ngawira na mateka. Wakati wa kurejea kwao huku, wakapita kwenye ngome za Al-Haarith Ibn Muawiyah (hawa ni miongoni mwa wale walio ipinga faradhi ya Zakah). Miongoni mwao alikuwemo Ash-ath Ibn Qays, huyu akaja akawanyang’anya Waislamu mateka wao. Gavana Ziyaad akachukua hatua za haraka kwa kumuandikia waraka wa kumuita haraka Al-Muhajir  Ibn Abi Umayyah; gavana wa Baniy Muawiyah wa Kandah. Al-Muhajir akampa ukaimu wa jeshi lake Ikrimah na yeye akatoka wangu wangu na watu wake mpaka akafika kwa Ziyaad. Wote kwa pamoja wakayaunganisha majeshi yao na kupambana vikali na waritadi wale. Baniy Al-Harith wakashindwa vibaya, wakakimbia na kwenda kujificha Najeer; hii ni ngome yao. [Rejea AT-TWABAQAATUL-KUBRAA 6/22]

Waislamu wakawazingira, mzingiro ulipo shitadi na hali kuwa ngumu, waliamua kutoka ngomeni na kupambana mpambano ambao haukuwafaa kwa lolote. Wakalazimika kurudi tena kujificha ngomeni, kisha ndipo As-ath akamtuma mjumbe kwa Waislamu kutaka kufanya nao suluhu. Katika suluhu hiyo, wao wataisalimisha ngome hiyo na vyote vilivyomo humo kwa Waislamu, kwa sharti la kupewa amani kwa viongozi tisa. As-ath akaandika tamko la suluhu hii na akayaorodhesha majina ya viongozi anao taka wapewe amani na Waislamu, lakini akasahau kuliorodhesha jina lake mwenyewe. Waislamu wakaikubali suluhu hiyo, wakaingia katika ngome hiyo, wakawaua askari wapiganaji, wakachukua mateka na ngawira. Kisha wakaangalia orodha ya watu walio ombewa amani katika waraka wa suluhu, tahamaki jina la Ash-ath halimo. Al-Muhajir akataka kumuua, lakini wafuasi wake wakamshauri asimuue na badala yake ampeleke kwa khalifa Abu Bakri, yeye kama Amiri wa waumini ndiye aamue hatima yake. Akaukubali ushauri huo wa wafuasi wake na akampeleka kwa Sayyidna Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-nae akamsamehe na kumuacha huru. Ash-ath huyu baadae alikuwa ni miongoni mwa Waislamu walio onyesha ushujaa mkubwa katika ufunguzi wa Iraq.

Mpaka hapa, ewe ndugu mwema-Allah akurehemu-khabari za waritadi zinakoma. Kutokana na khabari hizi, Waislamu wanao taka kufuata nyayo za wahenga wao wema, wanapata somo kwamba muumini hatakiwi kuwa dhalili vyovyote watakavyo kuwa wengi maadui zake. Kwa sababu Waislamu hawashindwi kwa sababu ya uchache wao na wala hafedheheki ila ni kwa kufuata kwao matamanio maovu ya nafsi zao. Na kwa sababu ya kukengeuka kwao, wakaacha kuifuata njia ya sawa.

Huyu hapa Sayyidna Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-khalifa wa kwanza wa Waislamu. Waarabu wote walikuwa dhidi yake, maadui zake, basi akawa yeye na wote walio kuwa pamoja nae ni kama mwenge angavu ndani ya pango lenye kiza totoro. Basi hilo la kuwa na mahasimu kila pembe, halikumzuia yeye pamoja na Waislamu walio simama nae imara kuitukuza dini ya Allah na kupigana na wale walio mkufuru Allah. Bali aliamini kwa yakini kabisa ahadi ya Allah pale alipo sema: “ENYI MLIO AMINI! MKIMNUSURU ALLAH NAE ATAKUNUSURUNI NA ATAITHIBITISHA MIGUU YENU”. [47:07] – Yaani mkiinusuru dini ya Allah, na Yeye atakunusuruni muwashinde maadui zenu na ayatilie nguvu mambo yenu.

Kwa imani yake hiyo, Allah Ataadhamiaye akamlipa kwa kumpa nusura adhimu dhidi ya maadui zake na ushindi mkubwa akaupata, Uma wote wa Kiarabu ukawa chini ya utii wake. Hivyo ndivyo unavyo kuwa Uislamu na Imani, tanabahi na uzingatie!

 

 III.       Suala (kadhia) la Iraq:

         Sayyidna Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-alipo maliza kuwashughulikia waritadi na kufanikiwa kuwakusanya Waarabu wote chini ya Uislamu na Allah akalifanya neno lao kuwa moja. Akaielekeza hima yake katika kuuneza uadilifu na usawa wa Uislamu miongoni mwa mataifa mengine. Ambayo wafalme wake walikuwa wakiitakidi kwamba wao wako katika daraja ya juu kuliko raia zao. Kwa itikadi yao hii, wakawasawirisha fikirani/akilini mwao kuwa ni watumwa wao wasio na mamlaka yoyote na nafsi zao. Natija ya taswira ovu hii ikawa ni kuamiliana nao kwa dhuluma na jeuri kubwa.

Tawala/falme kubwa zilizo jiranikiana na Dola ya Kiislamu enzi hizo, ulikuwa ni ufalme wa Fursi kwa upande wa Mashariki na ufalme wa Urumi kwa upande wa Kaskazini. Akaamua kuanza na Fursi na tukio la mwanzo lililo tokea baina ya Waislamu na dola hii kubwa, ni ule waraka wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alio muandikia Kisraa (mfalme) Abrawiyzi akimlingania Uislamu. Kisraa akauchana chana waraka huo wa Mtume kwa ujivuni, jeuri na kiburi. Kitendo chake hiki kinakuonyesha kiwango cha jeuri na kiburi topea ambavyo ndivyo vilikuwa nembo ya wafalme enzi hizo, dini ya haki ikaja kuyaondosha mambo mabaya haya. Jeuri ya Abrawiyzi kwa waraka huu wa Mtume, ilimfikisha kumpa amri gavana wake wa Yemen; Baadhaan atume watu wawili mashujaa, weledi wa vita wakamkamate na kumleta mbele yake Mtume. Gavana akaipokea amri hiyo, akawatuma watu wawili nao wakaenda kama walivyo amrishwa. Watu wawili hao walipo fika Madinah, walipokelewa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-akawaambia: “Leo ameuawa Abrawiyzi, ameuawa na mwanawe”. Na hali ikawa kama alivyo ieleza Mtume wa Allah, kwani Shairawaihi alimpindua kwa msaada wa wakuu wa Fursi, akamuua na kukalia kiti cha ufalme wa Fursi. [Rejea AL-BIDAAYATU WAN-NIHAAYAH 4/269].

Watu wawili hao walipo tambua kuwa ni kweli maneno waliyo ambiwa na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-wakasilimu. Na Shairawaihi (Kisraa mpya) akamtumia ujumbe gavana Baadhaan ya kwamba asimbughudhi Mtume wa Allah.

Na katika zama zake Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-nchi ya Yemen ilifunguliwa na Baadhaan akasilimu, hapo Mtume akamtawaza kuendelea kuwa gavana wake. Yemen ikawa ndio nchi ya kwanza iliyo kuwa chini ya himaya ya Fursi, kujiunga na Uislamu. Kisha zikafuatia baada yake Bahrein na Oman ambazo nazo pia zilikuwa chini ya Fursi. Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alipo fariki na khalifa Abu Bakri kumaliza kupambana na waritadi. Akamteua Sayyidna Khalid Ibn Al-Waleed; panga la Allah kuwa mtu wa kwanza atakaye asisi misingi ya dini nyoofu katika nchi za Fursi. Uteuzi huu ulifanyika mwanzoni mwa mwezi wa Muharram (Mfunguo nne) wa mwaka wa 12 Hijiria. [Rejea AL-BIDAAYATU WAN-NIHAAYAH 4/739 na TAARIKHUT-TWABARIY 2/332].

Na akamuamuru kuanza na Ubullah (mojawapo ya ngome za Fursi iliyo kuwa katika Ghuba ya Kiarabu kwenye maporomoko ya mto Dajlah) na akamuongezea nguvu kwa kumpa msaidizi, Al-Qa’aqaa Ibn Amrou. Na akamteua Iyaadhw Ibn Ghanam kuishambulia Fursi kwa kutokea Kaskazini mwa Iraq na akamuamuru kuanza na Muswayakh (kijiji kilicho kuwa pembezoni mwa mto Furaat, Kaskazini mwa Iraq). Na akamuongezea nguvu kwa kumpa usaidizi wa Abdi Yaghuuth     Al-Humeiriy, akawaamuru kuwatolea wito wa kutoka pamoja nao, wale walio pigana na waritadi. Na kwamba wasishirikiane pamoja na waritadi, kwani maoni yake Khalifa Abu Bakri-Allah amuwiye radhi-yalikuwa ni kutotaka msaada wa kijeshi kwa mritadi.

 

 



 | Tuandikie |