|
SOMO LA KUMI NA MOJA.
i.
Hurmuzaan abatilisha
(aacha kuheshimu) mipaka iliyo wekwa:
Baada ya suluhu na kuandikwa kwa mkataba wa amani
baina ya mshindwa; Hurmuzaan na washindi Waislamu kwa masharti yaliyo wekwa
na Waislamu. Hurmuzaan aliacha kuendelea kuuheshimu mkataba huo, kwa sababu
ya kutokuelewana katika uwekwaji wa mipaka kuliko tokea baina yake na wale
walinzi wa ngome ya Manaadhir na ile ya mto Tairi. Hurmuzaan akaomba msaada
kwa Wakurdi, wamsaidie kumaliza udhia wa Waislamu. Gavana wa Basra; Utbah
akamwandikia waraka Amirul-Muuminina kumfahamisha hali ya mambo ilivyo, ili
kupata maelekezo ya nini cha kufanya kutoka kwake. Sayyidna Umar akampa
Utbah idhini ya kwenda kukabiliana na mpinzani/muasi huyu. Na akawaongezea
nguvu Waislamu kwa kuwapa Hurquusw Bin Zuhair As-sa’adiy na akamfanya kuwa
ndiye amiri jeshi atakaye ongoza mapambano. Na ndiye awe mtawala wa maeneo
yote atakayo yatwaa kutoka kwa Hurmuzaan. Akaenda na likasonga mbele pamoja
nae jeshi la Basra mpaka wakafika katika daraja la soko la Al-Ahwaaz.
Wakavuka daraja, wakapambana na Hurmuzaan mpaka wakamshinda, akaponyoka na
kukimbia. Amiri Hurquusw akampa Juz’uu Bin Muawiya jukumu la kumfuatilia
haini huyu mpaka atiwe nguvuni. Akaenda, akafanikiwa kulikomboa soko la
Al-Ahwaaz, lakini kwa mara nyingine tena Hurmuzaan akaponyoka. Akaelekea
kwenye mji wa Souq; makao makuu ya jimbo la Al-Ahwaaz, akaukomboa na
akawatolea wito wale walio kimbia kurejea kwenye mkataba na watoe kodi,
wakakubali. Akakaa hapo akiwa ndiye liwali kama alivyo ambiwa na Sayyidna
Umar, akauamirisha mji, akachimba mito na akahuisha ardhi nyifu mpaka ikafaa
kwa kilimo.
Halafu yake, Hurmuzaan akaandikiana na liwali Hurquusw
akitaka kupewa nafasi ya kufanya suluhu kwa mara nyingine tena. Hurquusw
akamkubalia ikiwa ni baada ya kuomba ruhusa kutoka kwa Sayyidna Umar.
Hurmuzaan akaishi chini ya himaya ya Waislamu, nao wakimuhami dhidi ya
Wakurdi. Liwali Hurquusw akapiga kambi kwenye mlima Al-Ahwaaz, hilo
likawawia uzito Waislamu na Ahlud-dhima. Habari zikamfikia kiongozi mkuu;
Sayyidna Umar, akamwandikia waraka akimuagiza kushuka kwenye ardhi tambarare
na kwamba asimfanyie uzito muislamu yeyote wala mtu mwenye dhima. Na ya
kwamba usimpate unyong’onyevu wala haraka, asije akaitia vunju Dunia yake na
hiyo ikawa ndio sababu ya kuikosa Akhera yake.
Na ni ndani ya kipindi hiki ndimo Sayyidna Umar alifanya
mabadiliko ya uongozi wa Basra. Akamteua Al-Mugheera Bin Shu’ubah kuwa
gavana mpya wa Basra, kufuatia kifo cha gavana wake wa kwanza; Utbah Bin
Ghazwaan-Allah amuwiye radhi. Baada ya muda akamuuzulu (akamvua madaraka) na
kumteua Abu Mousa Al-Ash’ariy kushika nafasi yake. Na akampa wasaidizi
ishirini na tisa katika maswahaba wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie. Miongoni mwao alikuwemo Anas Bin Maalik, Imraan Bin Huswein na
Hishaam Bin Aamir.
Katika enzi za ugavana wa Abu Mousa, alikuwa Yazdajrid;
mfalme wa Fursi akipita huku na huko akiwatolea Wafursi wito wa kumnusuru na
kuurejesha ufalme wao. Wakafanya harakati, wakawaandikia watu wa Al-Ahwaaz
ambao Hurmuzaan alifanya suluhu kwa niaba yao. Khabari zikawafikia maliwali
wa Al-Ahwaaz, nao bila ya ajizi wakampelekea ujumbe Sayyidna Umar. Sayyidna
Umar akamwandikia waraka Sa’ad; gavana wa Koufah akimuagiza kupeleka
haraka Al-Ahwaaz jeshi kubwa liongozwe na Noumaan Bin Muqarrin. Na
akamwandikia waraka Abu Mousa; gavana wa Basra nae apeleke jeshi kubwa
kwenda huko chini ya uongozi wa Muaddi Bin Aliy. Na kamanda wa majeshi yote
mawili; lile la Koufah na la Basra awe ni Abu Sabrah Bin Abi Ruhmi. Basi
Noumaan Bin Muqarrin akasonga mbele na jeshi lake mpaka akafika
Raamahurmuzi; mji katika Khuzistaan na akamkuta humo muasi Hurmuzaan.
Noumaan akapambana nae mpaka akamshinda na akautwaa mji huu.
ii.
Ushindi wa Tustar:
Jeshi la Basra lilipo fika Al-Ahwaaz, likapiga
kambi katika soko la Al-Ahwaaz na walikuwa wanataka kuelekea Raamahurmuzi.
Ndipo ikawafikia khabari ya tukio lililo tokea na kwamba Hurmuzaan
amekimbilia Tustar, wakamfuata huko. Noumaan na maliwali wa Al-Ahwaaz
nao wakaelekea huko, wote wakafika na kukuta Wafursi wamechimba handaki
kuzunguka mji. Waislamu hawakuwa na la kufanya ila kuuzingira mji huo.
Miongoni mwa watu walio onyesha ushujaa mkubwa katika mzingiro huu, walikuwa
ni Al-Baraau Bin Maalik, Maj-zaa Bin Thaur na idadi kadhaa ya mujahidina
walio toka Basra na Koufah.
Mzingiro ulipo wahemeza watu wa Tustar, akatoka mtu mmoja
miongoni mwao akawaomba amani Waislamu kwa sharti ya kwamba awafahamishe
njia watakayo weza kuitumia kuingia mjini. Waislamu wakampa amani, nae
akawafahamisha njia iliyo katika maji. Kamanda wa jeshi akahamasisha watu
watakao fuatana na mtu yule kupita katika njia hiyo. Akaitikiwa na idadi
kadhaa ya mujahidina wa Basra na Koufah, wakaingia kwenye hiyo njia ya chini
ya maji (tunnel). Huku Waislamu wakisubiri kwa hamu kubwa kusikia takbira
yao itakayo ashiria kwamba tayari wameshaingia ndani ya mji. Walipo ingia
wakapiga takbira na Waislamu wakaipokea takbira yao hiyo, milango ya mji
ikafunguliwa na aliye jaribu kupigana aliuawa.
Ama Hurmuzaan yeye alijifungia ndani ya ngome ya mji,
wakamzunguka. Alipo ona hana hila, akawaomba Waislamu wamruhusu kutoka kuja
kukabiliana na hukumu itakayo tolewa na Amirul-Muuminina; Sayyidna
Umar-Allah amuwiye radhi. Waislamu wakamkubalia na kadhia yake wakaiacha
mikononi mwa Sayyidna Umar. Katika mzingiro huu, aliuawa Al-Baraau Bin
Maalik na Maj-zaa Bin Thaur.
iii.
Ushindi wa Suus:
Baada ya ukombozi wa Tustar, hiloo jeshi la haki
likasonga mbele mpaka likafika Suus; sehemu katika jimbo la Al-Ahwaaz,
wakaufungua mji huu kwa suluhu. Kisha amiri jeshi akapeleka sariya (kikosi
kidogo) kwenda kuufungua mji wa Jundisaabour, wenyeji wake wakafanya nao
suluhu. Baada ya kukamilika kwa ufunguzi wa miji, Abu Sabrah; kamanda wa
jeshi la Basra akampelekea Sayyidna Umar wajumbe, miongoni mwao alikuwemo
Al-Ahnaf Bin Qays na Anas Bin Maalik wakiwa pamoja na haini Hurmuzaan.
iv.
Ujumbe wa Hurmuzaan:
Walipo fika Madina, makao makuu ya dola ya Kiislamu
chini ya khalifa wa pili wa Mtume; Sayyidna Umar Bin Al-Khatwab-Allah
amuwiye radhi. Wakamvika Hurmuzaan vazi lake rasmi la hariri ambalo
limenakishiwa kwa dhahabu na wakamvika na taji lake la ufalme ambalo
lilikuwa limetiwa vipambo vya yakuti. Walifanya hivyo ili Sayyidna Umar na
Waislamu wapate kuiona fahari ya Wafursi. Baada ya kumvika vazi lake rasmi
hilo, haoo wakaelekea msikitini aliko kuweko Amirul-Muuminina, wakamkuta
amelala chini. Hurmuzaan akauliza: Yu wapi Umar? Wakamjibu: Huyoo hapo aliye
lala chini. Akauliza tena: Wako wapi walinzi na wapambe wake? Wakamjibu:
Hana walinzi wala wapambe. Akasema: Basi huyu atakuwa mtume (sio
mtawala/kiongozi). Wakamwambia: Kamwe si Mtume, ila anatenda (anafuata)
matendo ya mitume.
Sayyidna Umar akaamka, akaambiwa ujio wa Hurmuzaan,
akamuangalia na kusema: “Sifa zote njema zinamstahikia Allah ambaye
ameudhalilishia Uislamu mtu huyu na walio kama yeye”. Kisha akaamuru avue
vazi hilo la fahari na badala yake avae nguo za kawaida kama watu wengine.
Halafu tena Sayyidna Umar akamuuliza haini huyu: Umeyaonaje matokeo ya
kuvunja ahadi na mwisho wa amri ya Allah? Akasema: Ewe Umar! Sisi na nyinyi
katika zama za jahiliya Allah alituacha wenyewe, tukakushindeni. Sasa mlipo
kuwa na dini, mmetushinda. Sayyidna Umar akamwambia: “Hakika si kwa
jinginelo, nyinyi mlitushinda katika zama za jahiliya kwa sababu ya umoja
wenu na utengano (utapanyi) wetu”.
Kisha Sayyidna Umar akamuuliza: Nini hoja yako na nini
udhuru wako katika kuvunja suluhu mara baada ya mara? Akasema: Ninachelea
usije ukaniua kabla sijakueleza. Sayyidna Umar akamwambia: Usilikhofu hilo.
Akaomba maji, akaletewa katika hero (bilauri ya mbao), akasema: Bora kufa
kwa kiu kuliko kunywa maji katika chombo kama hicho. Akaletewa maji katika
chombo anacho kipenda, akasema: Ninachelea kuuawa kabla sijayanywa maji.
Sayyidna Umar akamwambia: Hutafikwa na baya lolote mpaka umalize kunywa.
Akamtoa shaka/wasiwasi, akawa na amani. Sayyidna Umar akasema: Muongezeeni
na wala msimkusanyie pamoja kuuawa na kiu. Akasema: Sina haja ya maji,
hakika si vinginevyo nilitaka tu yawe sababu ya kupatia amani. Sayyidna Umar
akamwambia: Sasa nataka nikuue. Akasema: Mbona umeshanipa amani? Sayyidna
Umar akamwambia: Mwongo wee! Anas Bin Maalik akasema: Amesema kweli, ewe
Amirul-Muuminina, umekwisha mpa amani. Sayyidna Umar akamwambia: Ewe Anas!
Mimi nimpe amani muuaji wa Al-Baarau Bin Maalik na Maj-zaa Bin Thaur,
inawezekanaje?! Wallah, utoe njia au nitakuadhibu! Akasema (Anas): Wewe
ulimwambia hutafikwa na baya lolote mpaka uniambie na wala hutafikwa na baya
lolote mpaka uyanywe maji. Na watu walio mzunguka nao wakasema hivyo hivyo.
Akamwendea Hurmuzaan akamwambia: Umenihadaa, wallah mimi sihadaiwi ila na
muislamu.
Hurmuzaan akasilimu na akawa miongoni mwa wawafuatao
maswahaba kwa wema (Taabiina). Sayyidna Umar akamwandikia kupewa kipawa/tuzo
ya elfu mbili. Al-Mugheerah Bin Shu’ubah ndiye aliye kuwa mkalimani baina
yao.
Kisha Sayyidna Umar akawageukia wajumbe, akawauliza: Huenda
Waislamu wanawafanyia maudhi watu wa dhima, ndio sababu wanavunja mkataba?
Wakajibu: Sisi hatujui kwao ila utekelezaji wa kila walilo likubali katika
mkataba. Akasema Sayyidna Umar: Kama msemavyo ndivyo, haya (ya uvunjaji)
yanatokeaje? Akasema Al-Ahnaf Bin Qays: Ewe Amirul-Muuminina! Bila ya shaka
wewe ndiye uliye tukataza kuingia ndani kabisa ya miji na hakika mfalme wa
Fursi bado yuko miongoni mwao. Kwa hivyo hawataacha kupigana vita nasi muda
wa kuwa mfalme wao yumo miongoni mwao. Na wala falme mbili (ndani ya nchi
moja) hazitawafikiana mpaka ufalme mmoja uutoe ule mwingine. Nawe umekwisha
ona kwamba sisi hatukutwaa sehemu ikifuatiwa na nyingine, ila ni kwa sababu
ya uasi wao na kutotekeleza kwao ahadi. Na hapana shaka kwamba mfalme wao
ndiye anaye watuma kufanya hivyo. Na hilo litaendelea kuwa ndio zoweo lao
mpaka utakapo tupa ruhusa ya kuingia ndani zaidi ya miji yao ili tuung’oe
ufalme wao. Hapo ndipo yatakapokatika matumaini yao na ndipo watakapo koma.
Akasema Sayyidna Umar: Wallah, umeniambia kweli. Na akatia azma ya kuufuata
ushauri wake.
|