|
SOMO LA KUMI NA TISA.
I/.
Sayyidna Uthman aasiwa.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa
akiutahadharisha umma wake dhidi ya kuibua na kuchochea fitina miongoni
mwake. Na ni mara nyingi tu alikuwa akitoa tahadhari dhidi ya fitina, kwa
sababu nguvu ya umma pale itakapo gurishwa kutoka kwa adui na kuletwa kwa
wana wa umma wenyewe, hali ya umma huo itakuwa ni mbaya na nidhamu/mpangilio
wake utafisidika. Na umma huo utakuwa karibu mno na uhovyo hovyo/fujo/ghasia
na mbali mno na utengefu/ukaa sawa/ushwari.
Na zimepokewa hadithi nyingi kutoka kwa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-katika kadhia nzima ya kutahadharisha juu ya
fitina. Lakini lililo kadiriwa na Muumba tangu azali kuwa, likawa/likatokea.
Funguzi (ushindi) zilikamilika kwa umma kama yalivyo kamilika mamlaka
(ufalme) na mipaka ya Dola ya Kiislamu ikatanuka kutokea Madina mpaka Koufa
(Iraq), Shaamu (Palestina) hadi Misri (Afrika). Na walio kuwa wakikhusika na
suhuba (uswahaba) ya Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-na wenye
kuufuata mwendo na taratibu zake, ni Makuraishi katika Muhajirina (wazalendo
wa Makka), Answaari (wazalendo wa Madina) na watu wa Hijaazi. Na wengineo
wachache walio bahatika kuipata fursa hiyo adhimu. Ama Waarabu wengine wa
makabila (koo) ya Bakri bin Waail, Abdil-Qaysi, wengine katika ukoo wa
Rabeeah, Azdi, Kandah, Tamim, Qudhwaah na wengineo, wote hawa hawakuwa na
daraja katika usuhuba huo ila wachache tu miongoni mwao. Lakini walikuwa na
mguu (mchango) katika funguzi za miji mbali mbali iliyo angukia mikononi mwa
Dola Adilifu ya Kiislamu. Wao wakawa wanaliona hilo wenyewe pamoja na ubora
walio upata wale maswahaba wa mwanzo kumfuata Mtume wa Allah. Mlango huo
ulipo dhibitika na hali ikasahaulika kidogo, adui akadhalilika na dola
ikazidi kuwa na nguvu. Hapo vishipa vya jaahiliya vikaanza kupiga na wakaona
uongozi wa umma umeshikwa na Muhajirina na Answaari katika Makureishi na
wengineo. Ndipo nafsi zikaingiwa na chuki na tamaa ya uongozi, na vuguvugu
baya hili likajitokeza katika enzi za ukhalifa wa Sayyidna Uthman-Allah
amuwiye radhi. Chokochoko zikaanza kwa magavana wake alio wateua kuongoza
majimbo mbali mbali, watu wakaanza kuwakataa na kudai waezuliwe na wateuliwe
magavana wengine wanao wataka wao na yakakithiri mno madai ya kumkataa
Sayyidna Uthman na uongozi wake.
II/.
Kiongozi wa fitina; Ibn
Sabai.
Kiongozi wa fitina hii kubwa kuwahi kuwakumba
Waislamu tangu kufariki kwa Bwana Mtume-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa ni
yule Muyahudi ambaye tulisha wahi kumtaja, aitwaye Abdullah bin Sabai. Huyu
alizuka na madai ya kumtetea Sayyidna Aliy bin Abi Twalib, akidai kwamba
yeye ndiye wasii wa Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. Akasema ni
nani dhaalimu zaidi kumshinda yule ambaye hakuupitisha wasia wa Mtume wa
Allah.
Basi wakayafuata madhehebu yake hayo na kuingia kwenye
mkumbo huo, wengi miongoni mwa watu bendera fuata upepo, ambao wana nyoyo
wasizo zingatia kwazo. Akawaambia: Lipiganieni jambo hili, kwani Uthman
ameutwaa uongozi pasina haki. Wakawaandikia watu wa majimboni, huko wakapata
waunga mkono wengi, wenye fikra kama za kwao, mpaka ukaenea uvumi wa
kulichafua jina la Sayyidna Uthman na magavana wake.
Khabari za uvumi na uzushi huo zikawafikia watu wa Madina,
wakamuendea Sayyidna Uthman kumuuliza na kupata uhakika wa suala hilo.
Sayyidna Uthman akawaambia: Sijapata khabari yoyote kuwahusu magavana wangu
ila ni salama tu, na nyinyi ndio washirika wangu na ndio mashahidi wa
waumini, basi hebu nipeni ushauri wenu. Wao wakamshauri ya kwamba atume
wapelelezi wake waende huko majimboni ili kupata undani na uhakika wa
khabari mbaya hizo. Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-akaupokea ushauri
wao huo kwa mikono miwili, akamtuma Muhammad bin Maslamah kwenda Koufa.
Usamah bin Zaid, yeye akapelekwa Basrah, Shaamu akatumwa Abdullah bin Umar
na Ammaar bin Yaasir akapelekwa Misri. Wajumbe wote wakarejea na kutoa
taarifa ya uchunguzi wao huko majimboni waliko tumwa, wakasema: Katika
upelelezi/uchunguzi wetu huko majimboni, hatukugundua ubaya wowote kwa
magavana wako. Isipo kuwa mjumbe Ammaar bin Yaasir aliye tumwa Misri, yeye
alifuatwa na kundi la wafuasi wa Ibn Sabai, wakamjaza maneno kwa upande wa
magavana wa Sayyidna Uthman na wakamzuia kurejea Madina. Abdullah bin Sa’ad
akamwandikia Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-kumjulisha juu ya kadhia
hiyo ya mjumbe wake. Sayyidna Uthman akapeleka ujumbe kwenye majimbo
mengine, ya kwamba ((Hakika mimi naanzisha utaratibu wa kuwaita kwangu
magavana wangu kila musimu wa Hijja, watu wa Madina wameniletea mashtaka ya
kwamba kuna watu wanao shutumu (tukana) na kuwapiga raia. Basi yeyote mwenye
madai katika hayo, na aje katika musimu achukue haki yake pale ilipo, kwangu
au kwa magavana wangu. Au toeni sadaka (kwa kusamehe), kwani hakika Allah
huwajazi (huwalipa) watoa sadaka)). [TAARIKHUT-TWABARIY 02/648]
Na akawatumia pia ujumbe magavana wake ya kwamba waje katika
musimu, wakaja kwake: Abdullah bin Aamir; gavana wa Basrah. Abdullah bin
Sa’ad; gavana wa Misri na Muawiyah bin Abi Sufyaan; gavana wa Shaamu.
Akawakusanya na akawaingiza katika kikao chake hiki na magavana wake,
mabwana Amrou bin Al-Aaswiy As-sahmiy, Saeed bin Al-Aaswiy
Al-Amawiy, na akawaambia (magavana wake mbele ya mashahidi alio waita): Ee
ole wenu nyie! Ni mashtaka na uvumi gani huu (unao nifikia juu yenu)? Mimi
nachelea isije kuwa watu wanasema kweli juu yenu, na hilo halifungamanishwi
ila nami (kwa kuwa ndiye niliye kuteueni). Wakamwambia: Kwani wewe hukutuma
wajumbe kwetu, je hukufikiwa na khabari kutoka kwa raia (tunao waongoza)?
Je, wajumbe wako hawajarejea, hawakuambiwa lolote na mtu yeyote? Wallah,
(wanao dai) hawakusema kweli na wala hawakutenda wema. Na wala sisi hatujui
msingi wa jambo hili na wala haifai kuusikiliza uvumi huu.
Baada ya kusikiliza majibu ya magavana wake juu ya tuhuma
walizo zushiwa, Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-akawataka ushauri katika
njia/namna ya kuituliza fitina ile. Ibn Aamir; gavana wa Misri akasema: Mimi
naona uwashughulishe na jihadi. Ibn Sa’ad; gavana wa Misri yeye akasema:
Mimi naona ufanye nao suluhu kwa kuwamegea fungu la mali. Muawiyah; gavana
wa Shaamu akasema: Mimi naona suala hili ulirejeshe mikononi mwa magavana
wao (wakamalizane nao huko majimboni mwao). Mmoja wa mashahidi, Ibn Aaswiy
akasema: Mimi naona wewe umekwisha wasikiliza (magavana wako) na umeridhika
(na maelezo yao) na umewazidishia zaidi ya alivyo kuwa akifanya (mtangulizi
wako) Umar. Basi mimi naona ufuate nyayo za sahibu wako, ukaze mahala panapo
hitaji mkazo (ukali) na uwe laini mahala panapo hitajia ulaini. Na akasema
Saeed: Pale atakapo angamia kiongozi wao, watu watatapanyika.
Sayyidna Uthman-Allah amuwiye radhi-akasema: Nimekwisha
usikia ushauri wenu nyote, nami nasema kila jambo linao mlango wa
kuliingilia. Hakika jambo hili ambalo linalo chelewa juu ya umma huu
litatokea/litakuwa na hakika mlango wake ambamo lilimo fungiwa, kabisa
utafunguliwa. Nasi tutaufunga kwa upole na maridhiano ila katika mipaka ya
Allah (hapo hatutakuwa na upole tena). Na iwapo ikiwa/kama utafunguliwa
mlango huo, basi hakuna yeyote atakaye kuwa na hoja dhidi yangu. Na Allah
amekwisha jua ya kwamba mimi sikuacha kuwanasihi watu kwa wema na hakika
jiwe la kusaga fitina linazunguka. Basi kheri na impate Uthman, iwapo
atakufa bila ya kulizungusha. Hebu watulizeni watu na wapeni bure haki zao.
Angalieni, zitakapo tiiwa haki za Allah basi msipakwe mafuta.
Kisha Sayyidna Uthman akafunga kikao kile cha dharura,
akaondoka na wakaondoka magavana kurudi majimboni mwao kuendelea na nyadhifa
zao. Gavana Muawiyah akafuatana na Sayyidna Uthman, kwa sababu njia ya
kurudi Shaamu inapitia Madina. Walipo fika Madina, Sayyidna Uthman-Allah
amuwiye radhi-akawakusanya maswahaba wakubwa. Muawiyah akasimama,
akamuhimidi Allah, kisha akasema: nyinyi ni maswahaba wa Mtume wa
Allah-Rehema na Amani zimshukie-na ni wateule wake katika viumbe wake nanyi
ndio watawalia wa mambo ya umma huu. Basi asiwe na tamaa ya huo (uongozi)
yeyote asiye nyinyi. Mlimchagua mtu wenu (mwenzenu Sayyidna Uthman) bila ya
kushurutishwa, wala si kwa tamaa (kupata kitu kutoka kwake). Naye amesha
kuwa mtu mzima na umri wake umekuwa mkubwa na lau mngeli msubiria (afikie)
ukongwe, basi angeli kuwa karibu mno (na hilo). Pamoja na kwamba mimi
ninatarajia Allah Ataadhamiaye kuwa ni Karimu mno kumfikisha katika umri huo
(wa ukongwe). Na yamesha enea maneno ya kuutoa (uongozi) kwenu nanyi
hamjalaumu kwa lolote katika hayo (maneno). Basi huu mkono wangu (naunga) na
wala msiwape watu tamaa katika jambo lenu (la uongozi wa umma). Naapa kwa
Allah, lau watautamani, hamtaona katu katika huo (uongozi) ila kurudi nyuma.
Sayyidna Aliy bin Abi Twaalib-Allah amuwiye radhi-akamkemea.
Sayyidna Uthman akasema: Amesema kweli mwana wa ndugu yangu, nami
nakwambieni kuhusu mimi na kile nilicho tawalishwa: Hakika sahibu zangu
(wenzangu) wawili walio nitangulia (Sayyidna Abubakar na Sayyidna Umar)
wamedhulumiwa nafsi zao kwa kuambiwa kuwa eti wamemdhulumu Sayyidna Aliy
ukhalifa), na mwenye kufuata njia yao ataraji ujira kutoka kwa Allah. Na
hakika Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie-alikuwa akiwapa jamaa zake,
nami niko katika kikundi cha watu masikini na uchache wa maisha. Basi nami
nikaukunjua mkono wangu kuchukua kitu katika hicho ambacho kitakacho nikimu.
Basi ikiwa mtaona kuwa hilo ni kosa, basi lirudisheni (lizuieni) fungu
(dogo) hilo, kwani amri yangu inafuata amri yenu.
Wakasema: Hakika umesibu (umefanya ndivyo khasa) na umetenda
wema. Umempa Khalid bin Useid elfu khamsini na Marwaan bin Al-Hakam elfu
themanini. Basi akatwaa hicho kutoka kwao, wakaridhia na wakaondoka wakiwa
radhi.
Kisha Muawiyah akaondoka kurejea Shaamu baada ya kumshauri
Sayyidna Uthman kuondoka naye, lakini hakukubali kwa ajili ya kutaka kuwa
karibu na Mtume wa Allah-Rehema na Amani zimshukie. [TAARIKHUT-TWABARIY
02/650]
Muawiyah akaenda na katika msafara wake akakipitia kikundi
cha Muhajirina, miongoni mwao akiwemo Sayyidna Aliy, Twalhah na Zubeir,
akawaambia: Nyinyi mmekwisha jua ya kwamba watu walikuwa wakiligombea jambo
hili mpaka Allah akamtuma Mtume wake na walikuwa wakizidiana ubora kwa
utangulizi (katika Uislamu) na utangu na jihadi. Basi ikiwa watalichukua
hilo (la uongozi), basi jambo hilo ni jambo lao na watu watawafuata. Na
ikiwa wanaitaka Dunia kwa kushindana, watapokonywa hilo na Allah
atalirejesha kwa watu wengine na Allah ni Muweza wa kuleta badali. Na hakika
mimi nimekuachieni mtu mzima, basi usianeni kumtendea wema na muungeni
mkono, mtanadi saada.
|